Swali: Kuna wanaosema kuwa imani ni kauli, I´tiqaad na ´amali. Lakini hata hivyo ´amali ni sharti ya kutimia kwa imani. Wanasema vilevile kuwa mtu hakufuru mpaka aamini. Je, hizi ni katika kauli za Ahl-us-Sunnah au hapana?

Jibu: Hii sio katika kauli ya Ahl-us-Sunnah. Ahl-us-Sunnah wanasema kuwa imani ni kauli, ´amali na I´tiqaad. Miongoni mwa kauli zao vilevile wanasema kuwa imani ni kauli ya ulimi, kauli ya moyo, matendo ya viungo na matendo ya kimoyo. Imani inakuwa kwa mambo haya.

Kauli ya ulimi ina maana ya kule kutamka. Kauli ya moyo ina maana ya kule kukubali na kusadikisha. Matendo ya moyo ina maana ya nia na Ikhlaasw. Na vilevile matendo ya viungo.

Miongoni mwa kauli zao vilevile wanasema kuwa imani ni kauli na ´amali. Wanachokusudia kwa kusema hivo ni kauli ya ulimi na ya moyo, na matendo ya moyo na ya viungo.

Miongoni mwa kauli zao pia wanasema kuwa imani ni kauli, ´amali na nia. Imani inakuwa kwa mambo haya; kauli za ulimi na za moyo, na ´amali za moyo na za viungo.

Haifia kusema kuwa matendo ni sharti ya kutimia [kwa imani]. Matendo ni sehemu ya imani. Hakusemwi kuwa matendo ni sharti ya kutimia. Hakusemwi vilevile kuwa matendo ni katika sharti [ya imani] au [matendo] yanailazimu [imani]. Haya yote ni katika maneno ya Murji-ah. Murji-ah wanasema kuwa matendo yanailazimu imani.

Ahl-us-Sunnah wanasema kuwa matendo ni sehemu ya imani. Hatujui kuwa kuna Ahl-us-Sunnah yeyote aliyesema kuwa matendo ni sharti ya kutimia [kwa imani].

Kuhusiana na kauli ya kusema kwamba mtu hawezi kukufuru mpaka aamini, hii ni kauli ya Murji-ah. Murji-ah ndio wanasema kuwa mtu hakufuru mpaka aamini. Wanasema vilevile kuwa matendo na maneno ni dalili juu ya I´tiqaad iliyomo ndani ya moyo. Hili ni batili. Kauli yenyewe ya kufuru kwa dhati yake ni kufuru. Kitendo chenyewe cha kikafiri kwa dhati yake ni kufuru. Allaah (Ta´ala) Amesema:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na alama Zake na Mtume Wake?” Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (09:65-66)

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://subulsalam.com/play.php?catsmktba=4735
  • Imechapishwa: 17/11/2014