ash-Sha´raaniy amesema:

“Vile ninavyoamini mimi na kila ambaye ana inswafu ni kwamba iwapo Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) angeliishi mpaka ikaandikwa Shari´ah yote na kukusanywa, angeichukua na kuachana na kila kipimo. Vipimo vingelikuwa vichache katika madhehebu yake kama ambavo vilevile vingelikuwa vichache katika madhehebu ya wengine. Lakini ilipokuwa kwamba dalili za Shari´ah ni zenye kutofautiana katika wakati wake pamoja na Taabi´uun na waliokuja baada ya Taabi´uun katika miji, vijiji na mipaka ya nchi, bila shaka ndipo kipimo kikawa ni chenye kutumika zaidi katika madhehebu yake ukilinganisha na madhehebu mengine. Kwa sababu madhebeu yake hayakuwa na dalili kutoka katika Qur-aa na Sunnah juu ya yale mambo ambayo yalitumia kipimo juu yake. Tofauti na ilivyokuwa katika madhehebu mengine. Wanachuoni walikuwa wamesafiri kwenda katika miji na vijiji kwa ajili ya kutafuta, kukusanya na kuziandika Hadiyth. Kwa njia hiyo ikawa Hadiyth za Shari´ah zinajazana zenyewe kwa zenyewe. Kwa hiyo hii ndio ilikuwa sababu ya kipimo kuwepo kwa wingi katika madhehebu yake na uchache katika madhehebu mengine.” (al-Miyzaan (1/62))

Sehemu yake kubwa imenakiliwa na Abul-Hasanaat katika ”an-Naafiy´ al-Kabiyr”, uk. 135, ambapo pia kaandika taaliki yenye kuisapoti na kuyaweka wazi zaidi. Arejee huko yule anayetaka.

Ikiwa huu ndio udhuru wa Abu Haniyfah kutokana na yale maoni yanayopingana na Hadiyth Swahiyh pasi na kukusudia (na bila shaka ni udhuru wenye kukubalika kwa sababu Allaah (Ta ´ala) haikalifishi nafsi zaidi ya vile inavyoweza), hivyo itakuwa haijuzu kumtukana kama wanavofanya baadhi ya wajinga. Ni wajibu kuwa na adabu naye. Kwa sababu ni mmoja katika maimamu wa waislamu ambao wameihifadhi dini hii na kuyasambaza mataga yake. Ni mwenye kulipwa thawabu kwa hali yoyote, ni mamoja amepatia au amekosea. Kama ambavyo haijuzu kwa wale wenye kumuadhimisha kushikamana na maoni yake yanayotofautiana na Hadiyth. Kwani Hadiyth ndio madhehebu yake, kama ulivyojionea mwenyewe akisema. Hawa wamoja wako mashariki na hawa wengine wako magharibi. Haki iko baina ya hawa wawili:

رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Ee Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo juu ya wale walioamini. Ee Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma, Mwenye kurehemu.” (59:10)

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 41-43
  • Imechapishwa: 18/01/2019