Haitoshi kubadilisha mada nyingine, ni lazima kukemea usengenyi

Swali: Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Yule anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho, basi aseme ya kheri au anyamaze.”[1]

Makusudio ni kwamba kwa mfano yuko kwenye kikao chenye usengenyi akae kimya na vinginevyo anashirikiana nao?

Jibu: Azungumze kheri kwa kukemea. Akiwasikia basi awazindue na kuwaambia wamche Allaah na waache usengenyi. Vivyo hivyo akiwa katika kikao ambacho kina usengenyi. Ikiwa kuna pombe awakataze nayo. Iwapo kuna uzinzi awakataze nayo. Namna hiyo ikiwa kuna maovu mengine ayakataze. Vinginevyo ajitenge na mahali hapo. Ajiweke mbali na asiketi nao kwenye maovu.

Swali: Au abadilishe mada?

Jibu: Ni lazima akemee maovu pamoja na kubadilisha mada. Ni lazima kukemea maovu:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu.”[2]

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa ulioteuliwa kwa watu – mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.”[3]

Ametanguliza kuamrisha mema na kukemea maovu kabla ya kuamini kutokana na ukubwa wa jambo.

Swali: Vipi wakati kwenye kikao kunakuwepo watu wazima ambapo inakuwa vigumu kuwaambia?

Jibu: Haki ni kubwa zaidi kuliko wao. Haki ni kubwa zaidi. Kwa ajili hiyo wakati ´Abdullaah bin ´Umar alipoona haya kuzungumza kuhusu mtende baba yake ´Umar alimwambia:

”Laiti ungelizungumza ingependeza zaidi kwangu kuliko kadhaa na kadhaa.”

Mtu asiidharau nafsi yake kutokana na kheri. Azungumze yaliyo na kheri na asimee maovu ingawa atakuwa mdogo wa watu.

[1] al-Bukhaariy (5672) na Muslim (47).

[2] 09:71

[3] 03:110

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/audios/2775/476-من-كتاب-الامور-المنهي-عنها
  • Imechapishwa: 10/11/2024