Haijuzu kumtii mtawala katika maasi au kuacha jambo la faradhi

Swali: Kuna kigezo kipi cha kumtii mtawala?

Jibu: Kigezo kilichopo ni kutomtii ikiwa atakuamrisha kumuasi Allaah. Kwa mfano anakwambia usiswali ya mkusanyiko, usiswali ila baada ya kutoka wakati, nyoa ndevu zako, kunywa pombe na mfano wa hayo hakuna kumsikiliza wala kumtii. Na ni wajibu kwa kila alieamrishwa maasi na mtawala kutomkubalia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Deni la Allaah lina haki zaidi ya kulipwa.”

Hukmu ya Allaah ina haki zaidi ya kufuatwa. Ama kitu ambacho si maasi ni wajibu kwa mtu kumtii mtawala. Na kumtii mtawala ni kumtii Allaah (´Azza wa Jall):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

”Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.” (04:59)

Tukisema kuwa si wajibu kwa mtu kumtii mtawala isipokuwa tu kwa yale mambo ambayo Allaah kaamrisha, kungelikuwa vurugu. Ama mawaziri, viongozi, wakuu na vichwa wa nchi; ni manaibu wa mtawala. Amri zao ni kama amri za mtawala. Wanatiiwa kwa yale amabyo si maasi kwa Allaah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (161 A) Tarehe: 1418-02-06/1997-06-12
  • Imechapishwa: 09/04/2022