Ramadhaan iliyobarikiwa iko mlangoni. Mwezi huu mtukufu ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameutukuza na akauchagua kati ya miezi mingine. Ameuchagua Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) na akaufadhilisha kwa fadhilah nyingi na sifa nyingi za kipekee. Miongoni mwazo:

1- Allaah (Ta´ala) amefanya funga yake ni faradhi miongoni mwa faradhi kuu za Uislamu. Bali kufunga Ramadhaan ni moja katika nguzo tano ambazo Uislamu hausimami wala kunyooka isipokuwa kwayo. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Uislamu umejengwa juu ya vitano; kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba tukufu ya Allaah.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanya kufunga Ramadhaan ni nguzo ya nne miongoni mwa nguzo za Uislamu.

2- Allaah (Ta´ala) amefanya kufunga Ramadhaan ni miongoni mwa sababu za kusamehewa madhambi na kupandishwa daraja. Amesema  katika Hadiyth Swahiyh:

”Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Kwa hivyo mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani, kwa matarajio hali ya kuridhia uwekwaji wake katika Shari´ah na si kwamba afunga kwa sababu ya kutaka kuonekana au kufuata kichwa mchunga, basi atapata thawabu hizi nyingi. Ni lazima yapatike masharti haya:

”Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Allaah (Ta´ala) amefanya kufunga Ramadhaan kunafuta makosa. Hata hivyo ni lazima kupatikane masharti haya; afunge kwa imani na kwa matarajio. Kwa msemo mwingine afunge kwa kutaka, kwa kupenda na kuridhia Shari´ah Yake.

3- Allaah (Ta´ala) ameweka katika Shari´ah kupitia Mtume wake kusimama na kuswali katika mwezi wa Ramadhaan. Amefanya kusimama usiku na kuswali ni miongoni mwa sababu za kusamehewa muda wa kuwa mtu atafunga kwa imani na kwa matarajio. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

”Mwenye kusimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Hii ni fadhilah kubwa.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Mwenye kusimam pamoja na imamu mpaka akaondoka, basi anaandikiwa kama ameswali usiku mzima.”

Mtu akiswali pamoja na imamu idadi ya Rak´ah zenye kuhesabika na asiondoke mpaka imamu aondoke, basi Allaah (Ta´ala) humwandikia kama amesimama usiku mzima. Hii ni fadhilah kubwa.

4- Miongoni mwa sifa za kipekee za Ramadhaan ni usiku huu mtukufu. Ni usiku uliyopo na wenye kuendelea katika mwezi wa Ramadhaan na unapatikana katika yale masiku kumi ya mwisho. Haya ndio maoni ya sawa. Baadhi ya wanachuoni wamesema kwamba umenyanyuliwa, lakini ni maoni dhaifu. Wengine wamesema kuwa unapatikana katika mwaka lakini haujulikani ni mwaka gani, lakini ni maoni dhaifu. Baadhi ya wengine wakasema uko katika mwezi wa Ramadhaan na haujulikani ni katika usiku gani, lakini ni maoni dhaifu. Maoni mengine yanasema kuwa uko katika mwezi wa Ramadhaan katika yale masiku kumi ya mwisho. Maoni sahihi ni kwamba unahamahama; mwaka huu unaweza kupatikana tarehe ishirini na moja, mwaka ungine tarehe ishirini na mbili, mwaka ungine tarehe ishirini na tatu, mwaka ungine tarehe ishirini na tano na kadhalika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Utafuteni usiku uliokadiriwa katika yale masiku kumi ya Ramadhaan.

Kuna uwezekano mkubwa wa kuupata katika zile nyusiku zinazoswaliwa Witr. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Utafuteni usiku uliokadiriwa katika Witr katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan.”

Haijulikani uko katika usiku gani. Hekima ya kuuficha ni kwamba waja wajitahidi katika kuyahuisha masiku haya kumi ya mwisho, wajitahidi kufanya matendo na kufanya ´ibaadah. Lengo ni ujira na thawabu zao ziwe nyingi.

Usiku wenye makadirio unahuishwa kwa kuomba du´aa, kumnyenyekea Allaah, kuswali, kutoa swadaqah na kulingania kwa Allaah kwa kuamrisha mema na kukataza maovu.

5- Matendo yanalipwa maradufu katika mwezi huu kama vile kisomo cha Qur-aan, kusema ”Subhaan Allaah”, kusema ”Laa ilaaha illa Allaah” na kusema ”Allaahu Akbar”.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://shrajhi.com.sa/uploads/rmadhan_02.mp3
  • Imechapishwa: 05/05/2019