Swali: Nakulalamikia moyo wangu kuwa msusuwavu na matendo mema kuwa magumu kwangu – je, kuna ufumbuzi? Aidha ni mwenye kupindukia juu ya nafsi yangu kwa maasi. Ni zipi nasaha zako kwangu na kwa dada zangu wasichana ambao tumeshughulishwa na mitindo na mfano wake miongoni mwa mambo ambayo yanamfitinisha kutokamana na dini yake?

Jibu: Ususuwavu wa moyo una dawa. Nayo ni kusoma Qur-aan kwa wingi. Dalili ya hilo ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

لَوْ أَنزَلْنَا هَـٰذَا الْقُرْآنَ عَلَىٰ جَبَلٍ لَّرَأَيْتَهُ خَاشِعًا مُّتَصَدِّعًا مِّنْ خَشْيَةِ اللَّـهِ

“Lau Tungeliiteremsha Qur-aan hii juu ya mlima, basi ungeuona ni wenye kunyenyekea wenye kupasukapasuka kutokana na khofu ya Allaah.”[1]

Mlima, kama tunavyotambua, jiwe ni kitu chenye uziwi. Lau Qur-aan ingeliteremka juu yake basi ungelikhofu na kutetemeka. Kadhalika moyo ukisoma Qur-aan ambapo mtu akasoma kwa mazingatio na kuelewa basi ni lazima imuathiri moyoni mwake. Sikiliza maneno ya Allaah (Ta´ala) katika Suurah “Qaaf”:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ

“Hakika katika hayo bila shaka ni ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye mwenyewe awe hadhiri.”[2]

Ee dada! Ni lazima kwako kusoma Kitabu cha Allaah kwa kukizingatia na kukhofu. Allaah atabadilisha ususuwavu huyu ulaini  na kurejea kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

Kuhusu wanawake wenye kujishughulisha na mitindo wamekhasirika duniani na Aakhirah. Isipokuwa akitaka Allaah. Utashangazwa na wanawake hawa ambao wameshughulishwa na mitindo wanazichosha nafsi zao, waume zao, wazazi wao na walezi wao.  Halafu pesa hizi zinaenda katika makampuni ambayo yanaleta mitindo hii. Huenda makampuni yenyewe ni makampuni ya kikafiri. Matokeo yake maadui zetu wanafaidika kwa pesa zetu wenyewe.

Ninawasihi wanawake na walezi wao wasiende nyuma ya mitindo hii isiyokuwa na kheri ndani yake zaidi ya kupoteza wakati na pesa. Aidha inaziathiri nyoyo katika kuikimbiza kutokamana na kumtii Allaah.

[1] 59:21

[2] 50:37

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (72) http://binothaimeen.net/content/1661
  • Imechapishwa: 17/08/2020