2925 – ´Abdullaah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) analala ilihali amesujudu, kulala kwake hakutambuliki isipokuwa pale anapokoroma. Halafu anasimama na kuendelea na swalah yake.”

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah katika ”al-Muswannaf” na kupitia kwake al-Baghawiy katika ”Sharh-us-Sunnah”: Ishaaq bin Mansuur ametuhadithia, kutoka kwa Mansuur bin Abiyl-Aswad, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Ibraahiym, kutoka kwa ´Alqamah, kutoka kwa ´Abdullaah.

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Wapokezi wake ni waaminifu na ni wapokezi wa al-Bukhaariy na Muslim isipokuwa tu Mansuur bin Abiyl-Aswad, lakini na yeye pia ni mwaminifu.

Ibn Abiy Shaybah pia ameihadithia pasi na Swahabah katika cheni ya wapokezi: Hushaym ametuhadithia, kutoka kwa Mughiyrah, kutoka kwa Ibraahiym ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilala katika msikiti mpaka akakoroma. Halafu akasimama na kuswali na wala hakutawadha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yalikuwa yanalala macho yake na wala haulali moyo wake.”

Kisha Ibn Abiy Shaybah na Ahmad wakasema: Wakiy´ ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Ibraahiym, kutoka kwa al-Aswad, kutoka kwa ´Aaishah aliyesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akilala mpaka anakoroma. Kisha anasimama na kuswali na wala hatawadhi.”

Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim. Kuhusu ziada ya Ibraahiym:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yalikuwa yanalala macho yake na wala haulali moyo wake.”

ni Swahiyh kwa cheni ya wapokezi ilioungana katika al-Bukhaariy na Muslim na kwenginepo. Nimeitoa katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (1212).

Ziada hii ni dalili ya wazi kabisa kwamba usingizi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) haukuchengua wudhuu´ wake na kwamba sifa hiyo ni maalum kwake yeye. Wanachuoni wametofautiana kama wudhuu´ wa aliyelala ambaye yuko imara katika ukaaji wake unachenguka au hauchunguki. Maoni yenye nguvu ni kwamba unachenguka, kama nilivyobainisha katika ”Tamaam-ul-Minnah”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (6/2/1027-1028)
  • Imechapishwa: 17/08/2020