Daktari wa kiume kufunua uchi wa mwanamke ili kujua aina ya maradhi anayouguwa


Swali: Ni ipi hukumu ya kufunua uchi wa mwanamke kwa sababu ya kutaka kujua maradhi? Ni ipi hukumu ya wanafunzi wa kike ambao hufunua nyuchi za wagonjwa wa kike kwa lengo la mafunzo?

Jibu: Kumfunua mwanamke yale ambayo analazimika kuyafunika kwa sababu ya maslahi ya matibabu kwa ajili ya kumbainishia maradhi alionayo ni jambo halina neno. Kwa sababu ni kwa sababu ya haja. Haja inafanya kufaa kitu kama hichi cha haramu. Kanuni inayojulikana ya wanachuoni inasema: yale yaliyoharamishwa uharamu wa njia unafanywa kufaa kwa haja na yale yaliyoharamishwa uharamu wa kidhati au kwa msemo mwingine uharamu wa malengo basi hayafanywi kufaa isipokuwa dharurah tu. Wakataja baadhi ya mifano ukiwemo mfano huu ambao ni kutazama yale ambayo hayafai kutazamwa kutoka kwa mwanamke kwa sababu ya haja. Ni kama ambavo mposaji anafaa kutazama yale ambayo hafai kuyatazama kwa sababu ya maslahi ya kuoa. Kadhalika mambo haya aliyouliza ndugu huyu. Inafaa kwa daktari wa kiume kumfunua mwanamke ili ajue maradhi na kumwambia sababu zake.

Swali: Ni ipi hukumu ya mwenye kuacha kusoma vyuo vikuu kwa sababu hiyo khaswa kwa kuzingatia kwamba endapo tutaacha kazi basi fungu litakuwa kwa wasiokuwa waislamu. Ni wanawake wa Kiislamu wangapi wameenda kwa wasiokuwa waislamu na natija mtoto tumboni akapuuzwa mpaka akafa na ovari zikaondoka kiasi cha kwamba hashiki mimba wakati mwingine. Tukiacha kazi ya udaktari ni nani atakayewatibu waislamu wa kike? Ni wengine isipokuwa ni maadui.

Jibu: Haijuzu kwa muislamu kuacha kusomea masomo ya udaktari kwa sababu ya jambo hili. Kwa sababu jambo hili, kama tulivyotangulia kusema katika jibu la kwanza, halina neno. Ikiwa halina neno basi haifai kwa mtu kuliacha kwa sababu ya mawazo anayofikiria na akadhania kuwa ni haramu.

Hapana shaka kwamba kujifunza udaktari ni faradhi kwa baadhi ya waislamu. Hivo ndivo walivosema wanachuoni. Kwa sababu mambo ya watu hayawezi kwenda isipokuwa kwayo. Jambo ambalo manufaa ya waislamu hayawezi kusimama isipokuwa kwalo basi litakuwa ni faradhi kwa baadhi ya watu japokuwa msingi wake sio katika mambo ya ´ibaadah. Kwa ajili hii wanachuoni wamesema katika kanuni zao zilizothibitishwa zilizoenea: manufaa yenye kuenea ambayo watu wanayahitajia inakuwa ni faradhi kwa baadhi ya watu. Mfano wa mambo hayo ni uhandisi, biashara, kufua vyuma na mengineyo. Wasipoyafanya watu wa kutosheleza basi inakuwa ni faradhi yenye kutosheleza kwa waislamu. Kujengea juu ya hili tunasema kuwa ni lazima kwa waislamu katika miji ya waislamu wajifunze kazi ya udaktari ili wajitosheleze na manaswara na wengineo.

Muulizaji: Hata kama hilo litapelekea katika yale wanayoona kuwa ni mazito katika kufunua nyuchi za waislamu na wengineo?

Ibn ´Uthaymiyn: Ndio, hata kama japo litapelekea kufunua nyuchi hizi.

Muulizaji: Wako baadhi ya wanafunzi wameacha kazi ya udaktari kwa sababu wanaona uzito kufunua nyuchi za waislamu.

Ibn ´Uthaymiyn: Sisi hatuoni hivo. Tunaona kuwa midhali jambo liko ndani ya ufaaji Kishari´ah basi haitakiwi kwa waislamu kuona uzito.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (09) http://binothaimeen.net/content/6725
  • Imechapishwa: 19/11/2020