Athari ya zakaah juu ya jamii na uchumi wa kiislamu

Swali: Zakaah ina athari gani juu ya jamii na uchumi wa kiislamu?

Jibu: Athari ya zakaah juu ya jamii na uchumi wa kiislamu iko wazi. Ndani yake kuna kuwafariji masikini na kusimamia maslahi ya ummah mzima. Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala)  amesema kuhusu jukumu la zakaah:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Hakika si venginevyo zakaah ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao [kwa ajili ya Uislamu] na kuwakomboa mateka na wenye deni na katika njia ya Allaah na msafiri [aliyeharibikiwa]. Ni faradhi itokayo kwa Allaah; na Allaah ni Mjuzi, Mwenye hekima.”[1]

Miongoni mwa aina hizi saba wako wanaoichukua kwa ajili ya kutatua shida zao na wengine wanaipokea kwa ajili ya waislamu wanaihitaji. Mafukara, masikini na wenye deni wanaipokea zakaah kwa ajili ya nafsi zao. Vivyo hivyo juu ya wasafiri na kuwakomboa mateka. Hawa wanaipokea kwa ajili ya nafsi zao. Wako wengine ambao wanaipokea kwa ajili ya watu ni wenye kuihitajia. Kwa mfano wa wale wapatanishi kati ya watu, wenye kuikusanya na wenye kupambana katika njia ya Allaah. Kwa hiyo tukishatambua kuwa zakaah inayoenda katika sampuli za watu hawa inaepelekea kutatua shida zao na waislamu wote kwa jumla wananufaika nayo, basi tutafahamu zakaah ina manufaa gani juu ya jamii.

Kuhusu upande wa uchumi, manufaa yake yanaenea kati ya matajiri na mafukara. Kiwango fulani cha mali ya mafukara inachukuliwa kwa ajili ya kupewa mafukara. Kwa njia hiyo kunpatikana mgawanyiko ili kuwepo usawa kati ya pande zote mbili.

Jamii pia inanufaika kwa namna ya kwamba watu wanakuwa na muungano. Mafukara wanapoona kuwa matajiri wanawapa pesa hizi, basi hapana shaka kwamba watawapenda wale matajiri na kutaraji yale ambayo Allaah amewafaradhishia katika kujitolea. Hali inakuwa tofauti pale ambapo wale matajiri wanapofanya ubakhili kwa zakaah yao. Kitendo hicho kinaweza kupelekea chuki na wale mafukara kuwa na uadui ndani ya nyoyo zao. Hilo limeashiriwa na mwishoni mwa Aayah tukufu ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema akibainisha manufaa ya zakaah:

فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

“Ni faradhi itokayo kwa Allaah; na Allaah ni Mjuzi, Mwenye hekima.”

[1] 09:60

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (18/12-13)
  • Imechapishwa: 19/05/2026