54. Hapa ndipo tutathibitisha ni nani atayeingia Peponi na Motoni

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Hatumshuhudii muislamu yeyote kwa kitendo alichofanya kuingia Peponi wala Motoni. Tunatarajia kwake mema na tunachelea kwake. Tunachelea kwa mtenda dhambi na tunatarajia kwake huruma ya Allaah.

MAELEZO

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema kuwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah hawamthibitishii yeyote kuingia Peponi pasi na dalili kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama vile Maswahabah kumi waliobashiriwa kuingia Peponi. ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Abu Bakr yuko Peponi. ´Umar yuko Peponi. ´Aliy yuko Peponi. Twalhah yuko Peponi. az-Zubayr yuko Peponi. ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf yuko Peponi. Sa´d bin Abiy Waqqaas yuko Peponi. Sa´iyd bin Zayd bin ´Amr bin Nufayl yuko Peponi. Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah yuko Peponi.”[1]

Riyaah bin al-Haarith amesimulia kuwa Sa´iyd bin Zayd bin Nufayl (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kutokana na yale niliyosikia kwa masikio yangu na kuyaelewa moyo wangu nashuhudia ya kwamba nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Abu Bakr yuko Peponi. ´Umar yuko Peponi. ´Aliy yuko Peponi. ´Uthmaan yuko Peponi. Twalhah yuko Peponi. az-Zubayr yuko Peponi. ´Abdur-Rahmaan yuko Peponi. Sa´d bin Maalik yuko Peponi. Muumini wa tisa yuko Peponi.” Ningelitaka kumtaja jina basi ningelimtaja jina.” Kukapowe uhai msikitini na kusemwa: “Ee Maswahabah wa Mtume wa Allaah! Ni nani huyo mtu wa tisa?” Akasema: “Mnaniuliza kwa jina la Allaah – na Allaah ni mkubwa. Mimi ndiye muumini wa tisa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye wa kumi.” Kisha akafuatisha kiapo na kusema: “Naapa kwa Allaah! Uso wa mtu ambao ulipatwa na vumbi akiwa bega kwa bega pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni bora zaidi kuliko matendo ya mmoja wenu ingawa ataishi umri mrefu kama wa Nuuh (´alayhis-Salaam).”[2]

[1] Ahmad (1/193), at-Tirmidhiy (3747) na Ibn Maajah (133). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (50).

[2] Ahmad (1/187).

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 134-135
  • Imechapishwa: 19/05/2026