Imaam at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hatumkufurishi muislamu yeyote kwa dhambi maadamu hakuihalalisha.”

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hatumkufurishi muislamu yeyote midhali hajafanya kitu chenye kutengua Uislamu. Haijalishi kitu ikiwa atazini, ataiba, atawaasi wazazi wake, atakata udugu na kadhalika. Tunasema huyu ni mtenda dhambi na amefanya dhambi kubwa. Imani yake ni yenye kupungua na dhaifu. Isipokuwa ikiwa kama atahalalisha kitu katika hayo hapo ndipo anakufuru. Kwa sababu katika hali hii atakuwa ni mwenye kumkadhibisha Allaah kwa kuharamisha zinaa, kuwaasi wazazi na kadhalika.

Jengine ni kwamba ni lazima hiki alichohalalisha iwe ni kitu kisichokuwa na tofauti kwa wanachuoni. Ima awe amekanusha kitu ambacho ni wajibu au ameharamisha kitu ambacho ni haramu. Kwa mfano apinge uwajibu wa swalah, zinaa, hajj au akahalalisha zinaa, kunywa pombe, ribaa au kuwaasi wazazi. Mwenye kufanya kitu miongoni mwa haya kwa kuyahalalisha, anakufuru. Ama akifanya na huku anakiri uwajibu wake au uharamu wake ikiwa kama ni haramu kweli, huyu ni mtenda maasi mwenye imani dhaifu. Amefanya dhambi kubwa. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/443)
  • Imechapishwa: 01/10/2020