Anayesikiliza mawaidha na darsa kupitia vyombo vya mawasiliano anapata thawabu na mwanamke mwenye hedhi kuingia msikitini?

Swali: Je, mtu anapata thawabu kwa kusikiliza Khutbah, mihadhara, nad-wah na vikao vya Dhikr kupitia redioni kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hawatokusanya watu katika nyumba miongoni mwa nyumba za Allaah wakisoma Kitabu cha Allaah, wakidarasishana baina yao, isipokuwa huteremkiwa na utulivu, hufunikwa na rehema na Allaah huwataja kwa wale walioko Kwake.”

Tunakusudia wanawake. Je, mwanamke anapata dhambi akiingia chini ya ngazi ya msikiti kwa upande wa ndani au ndani ya chumba chake ilihali yuko na hedhi kwa lengo la kusikiliza mawaidha na mihadhara?

Jibu: Kuhusu kipande cha kwanza hapana shaka kwamba mtu anapata thawabu kwa kusikiliza Qur-aan kupitia rekodi au redio. Vilevile anapewa thawabu kwa kusikiliza mawaidha, mihadhara na nad-wah zenye kunufaisha. Ni mamoja akafanya hivo kupitia redio au rekodi.

Miongoni mwa neema za Allaah (´Azza wa Jall) juu ya waja ni kupatikana kwa vifaa hivi vinavyorekodi yale wanayosema watu na vinawafikishia waliokaribu na waliombali. Lakini hawapati thawabu sawa na wale waliohudhuria ambao wanasoma Qur-aan. Kwa ajili hiyo iwapo tutaweka rekodi karibu na kipaza sauti ili iadhini badala ya mtu hakika kitendo hicho hakitofaa. Hii ni simbulizi ya adhaana na sio adhaana.

Kuhusu mwenye hedhi kuingia msikitini haifai. Isipokuwa kama ni kupita peke yake. Msikiti ni ile sehemu yote iliyozungukwa na ukuta. Ni mamoja ni ngazi au koridoo. Haijuzu kwake kubaki sehemu yote hii. Himdi zote ni za Allaah hivi sasa hakuna haja ya kufanya hivo. Kwa sababu anaweza kusikiliza kupitia kanda au kipaza sauti juu ya minara.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (61) http://binothaimeen.net/content/1392
  • Imechapishwa: 09/12/2019