67. Anakufuru anayepinga makadirio ya Allaah?

Kuna masuala: Wale wanaopinga mipango na makadirio wahukumiwe ukafiri? Wanachuoni walipambanua suala hili na wakasema ambaye atapinga ngazi ya kwanza – ambayo ni ya ujuzi – na akasema kuwa Allaah hayajui mambo isipokuwa baada ya kutokea kwake kwa njia ya kwamba pale yanapotokea ndio huyajua, mtu huyu anakufuru. Kwa sababu amepinga ujuzi wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Lakini hata hivyo wanasema kuwa wale wenye kupinga elimu wamekwisha. Hivi ndivyo alivyosema Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah”[1]. Mu´tazilah waliobaki wanathibitisha ujuzi wa Allaah (´Azza wa Jall) wa milele. Lakini hata hivyo wanapinga makadirio. Hivyo wao ni wapotevu. Hawafikii kiwango cha ukafiri. Kwa sababu watu hawa wanathibitisha elimu ya Allaah (´Azza wa Jall) na kuandikwa kwenye Ubao uliohifadhiwa. Wanachopinga ni utashi na matakwa. Bi maana wamethibitisha elimu na uandishi na wakachupa mipaka katika matendo ya waja na wakasema kuwa yanatokea pasi na utashi na matakwa ya Allaah (Jalla wa ´Alaa). Haya bado mpaka sasa yapo na yanaendelea kwa Mu´tazilah na yale mapote mengine yaliyochukua ´Aqiydah yao.

Huu ni ufupisho juu ya suala hili likubwa. Lakini inatosheleza kwa muislamu kuijua misingi hii na kusimama kwayo na wala asivuke mipaka katika kutafiti masuala ya mipango na makadirio. Asijifungulie juu ya nafsi yake mlango wa kuchukulia wepesi na kuzembea. Kwa sababu hatofikia natija yoyote. Kwa kuwa mipango na makadirio ni siri ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa waja Wake. Huwezi kufikia natija yoyote kwa kuchukulia wepesi na kuzembea. Ni juu yako kutembea pamoja na dalili za Qur-aan na Sunnah na uthibitishe mipango na makadirio na utambue dalili zake na hukumu ya mwenye kuyapinga.

[1] Tazama “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah”, uk. 164 kwa Sharh ya mtunzi (Hafidhwahu Allaah)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 153-154
  • Imechapishwa: 12/01/2024