Anafuta na kukibakiza akitakacho

Swali: Tunaomba tafsiri ya Aayah isemayo:

يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ

“Allaah anafuta yale ayatakayo na anathibitisha na Kwake ndiko kuna Mama wa Kitabu.”[1]

Je, ni Swahiyh Hadiyth isemayo:

يغفر ذنبًا ويفرج كربًا ويضع آخرين

”Anasamehe dhambi, anaondoa dhiki na anawashusha chini wengine.”

Hadiyth hiyo imetajwa katika mnasaba wa Aayah:

كُلَّ يَوْمٍ هُوَ فِي شَأْنٍ

”Kila siku Yeye yumo katika kuleta jambo.”[2]

Jibu: Ama maneno Allaah katika Aayah hii:

يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ

“Allaah anafuta yale ayatakayo na anathibitisha na Kwake ndiko kuna Mama wa Kitabu.”

Wanazuoni wamekhitalifiana katika kuifasiri. Baadhi yao wamesema kuwa maana yake ni yenye kuenea wenye kula khasara na wenye furaha. Baadhi yao wamesema kuwa maana yake ni maalum, nayo ni kwamba Allaah Anafuta apendacho katika hukumu za Shari´ah, kama yale yanayohusiana na yenye kufutwa na yale anayowateremshia Mitume Wake. Wengine wakasema kuwa maana yake ni kwamba Allaah anafuta apendacho miongoni mwa madhambi kwa kukubali tawbah na kusamehe. Aidha anaweka apendacho miongoni mwa mema. Allaah ndiye Mjuzi zaidi.

Kwa hivyo muumini anaweza kuichukua Aayah hii kwa ujumla wake na kumuomba Mola wake kila jambo linalomfaa. Akaomba tawfiyq, uongofu, awe miongoni mwa wenye furaha na si wenye kula khasara, akamuomba msamaha wa madhambi na faraja ya moyo na ufanisi katika matendo. Amwombe Allaah kila lenye kumnufaisha ulimwenguni na Aakhirah na atamani kupata baraka na rehema ya Aayah hii.

Ama masimulizi kuhusu maneno ya Allaah katika Aayah:

كُلَّ يَوْمٍ هُوَ فِي شَأْنٍ

”Kila siku Yeye yumo katika kuleta jambo.”

yamepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas kama maneno yake mwenyewe. Yeye amesema kuwa Allaah ana Kitabu anachokiangalia kila siku mara 360. Ndani yake huwapa baadhi ya watu utukufu, huwashusha wengine chini, huwafanya baadhi wafanikiwe na wengine wapate kinyume, huwainua juu watu na kuwateremsha chini wengine kwa hekima Yake. Masimulizi haya yamenukuliwa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas na maana yake ni sahihi.

[1] 13:39

[2] 55:29

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1100/معنى-قوله-تعالى-يمحو-الله-ما-يشاء-ويثبت
  • Imechapishwa: 17/02/2026