Swali: Kinachozingatiwa juu ya kuharibika kwa Swawm ya mwanamke mwenye hedhi ni kuzama kwa jua au kusikia adhaana? Je, mwanamke akipata hedhi baada ya kuhakikisha jua kuzama kisha baada ya hapo akasikia adhaana Swawm yake imeharibika au hapana?

Jibu: Kinachozingatiwa sio adhaana ya muadhini, bali kinachozingatiwa ni yale yaliyowekwa na Shari´ah na kufungamanisha hukumu kwacho. Kusimamisha kula ni pale inapobainika kuwa alfajiri imeingia. Allaah (´Azza wa Jalla) Anasema:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ

“Kuleni na kunyweni mpaka ibainike kwenu weupe [wa alfajiri] kutokana na weusi [wa usiku].” (02:187)

Hakusema:

“Mpaka Fajr iingie.”

Tazama ibara zilivyo! Kuna tofauti kati ya kubainika na kuingia. Hata kama alfajiri itaingia na wewe ukawa hujabainikiwa [hujawa na uhakika] hujakuwa na kitu juu yako. Ni lazima ibainike. Lakini hata hivyo mnielewe vizuri, haina maana namaanisha ya kwamba ukae chumbani mpaka mchana ukuingilie. Kwa kuwa huyu ambaye amekaa chumbani ni lini alfajiri itambainikia? Pengine wakati wa Dhuhr. Makusudio yangu sio haya. Makusudio yangu ni mahala kama nchikavu ambapo hakuna umeme na mtu akawa haijambainikia Subh, katika hali hii endelea kula na kunywa hata ikiwa waadhini wote wataadhini. Pamoja na hivyo, leo kwa vile watu wamekuwa hawawezi kutoka nje na kuangalia alfajiri ndio wakawa wanategemea adhaana. Lakini adhaana inayozingatiwa ni ile ambayo inaadhiniwa kunapoingia alfajiri…

Hali kadhalika, kinachozingatiwa ni kuzama kwa jua au adhaana? Ni kuzama kwa jua. Jua likizama hata kama watu watakuwa hawajaadhini, kula na kunywa. Upande mwingine, lau watu wataadhini na kukawa hakujazama, usile na kunywa. Kinachozingatiwa katika kukata Swawm ni kuzama kwa jua. Kinchozingatiwa katika kusitisha kula na kunywa ni kubainika kwa alfajiri.

Hivyo basi, mwanamke akipata hedhi baada ya kuzama kwa jua na kabla ya adhaana, Swawm yake ni sahihi. Upande mwingine, akipata hedhi baada ya adhaana lakini kabla ya kuzama kwa jua, Swawm yake imeharibika.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kanda “Liqaa´aatu Ramadhwaaniyyah”, sehemu ya 02
  • Imechapishwa: 23/09/2020