Aliye na janaba kufanya Tayammum licha ya kuwepo maji

Swali: Je, inajuzu kwa mwanaume ambaye ana jukumu la kuoga janaba kufanya Tayammum na kuacha kuoga ilihali maji yapo kwa hoja kwamba akijitakasa kwa kuoga atakosa swalah ya mkusanyiko na huku wakati wa swalah hautompita?

Jibu: Ikiwa ana jukumu la kuoga janaba, basi aoge wala hafanyi Tayammum. Haijuzu kwake kufanya Tayammum. Bali Tayammum hubatilika ikiwa maji yapo na anaweza kuyatumia maji. Inamlazimu kuoga hata kama atakosa swalah ya mkusanyiko. Ikiwa ikitokea kwamba akioa atakosa swalah ya mkusanyiko na akifanya Tayammum hatakosa swalah ya mkusanyiko, hapaswi kufanya Tayammum. Anaoga kwa maji na anaswali, hata kama ataswali nyumbani iwapo hatowahi swalah ya mkusanyiko.

Lakini ni wajibu kwake kupanga muda wa kutosha, kurekebisha saa yake kwa muda mpana au awaambie wanaomwamsha kabla ya alfajiri ili aweze kuoga na kuswali pamoja na mkusanyiko. Asiwe mlegevu. Watu wana saa; sasa saa zimerahisishwa. Aipange kwa wakati unaofaa ili aamke mapema, aoge kwa utulivu, aswali alichoandikiwa na Allaah, kisha aelekee kuswali swalah ya jamaa. Huu ndio wajibu wake. Tunamuomba Allaah atupe salama.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1871/حكم-تيمم-الجنب-مع-وجود-الماء-لكي-يدرك-الجماعة
  • Imechapishwa: 04/07/2026