Nilishangazwa wakati nilipohamishwa Makkah. Yemen nilikuwa na walinzi wanne mlangoni. Licha ya hivo hatukuwa na amani nyumbani kwetu si wakati wa usiku wala mchana. Nilikuwa naishi hotelini Daar-ul-Azhar Makkah. Baadhi ya nyusiku sipati usingizi na hivyo natoka kwenda Haram peke yangu. Ilikuwa katikati ya usiku. Nahisi neema, raha na ladha isiyo na kifani. Natoka nyumbani peke yangu. Amani hii sijawahi kuihisi katika nchi nyingine yoyote. Hilo sababu yake ni kwa kuwa watawala na wananchi wengi wameshikamana na Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mola wetu (´Azza wa Jall) amesema kweli pale aliposema kuhusu watu wa Kitabu:

وَلَوْ أَنَّهُمْ أَقَامُوا التَّوْرَاةَ وَالْإِنجِيلَ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْهِم مِّن رَّبِّهِمْ لَأَكَلُوا مِن فَوْقِهِمْ وَمِن تَحْتِ أَرْجُلِهِم ۚ مِّنْهُمْ أُمَّةٌ مُّقْتَصِدَةٌ ۖ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ سَاءَ مَا يَعْمَلُونَ

”Iwapo wangeliisimamisha vyema Tawraat na Injiyl na yale yaliyoteremshwa kwao kutoka kwa Mola wao, basi bila shaka wangelikula kutoka juu yao na kutoka chini ya miguu yao. Miongoni mwao lipo kundi la watu walioko katika njia ya sawa isiyopindukia na wengi wao wanayoyafanya ni mabaya mno.”[1]

وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَىٰ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِم بَرَكَاتٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ

”Na lau kama watu wa miji wangeliamimi na wakamcha Allaah, basi Tungeliwafungulia baraka tele kutoka mbinguni na ardhini.”[2]

وَقَالُوا إِن نَّتَّبِعِ الْهُدَىٰ مَعَكَ نُتَخَطَّفْ مِنْ أَرْضِنَا ۚ أَوَلَمْ نُمَكِّن لَّهُمْ حَرَمًا آمِنًا يُجْبَىٰ إِلَيْهِ ثَمَرَاتُ كُلِّ شَيْءٍ رِّزْقًا مِّن لَّدُنَّا

”Wakasema: ”Tukifuata mwongozo pamoja nawe, tutapokonywa kutoka ardhi yetu.” Je, kwani Hatukuwamakinisha Haram Tukufu na ya amani ambapo huletewa mazao ya kila kitu kuwa ni riziki kutoka Kwetu?”[3]

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا حَرَمًا آمِنًا وَيُتَخَطَّفُ النَّاسُ مِنْ حَوْلِهِمْ

”Je, hawaoni kuwa hakika Sisi Tumeifanya Haram kuwa ni Tukufu na yenye amani na huku wananyakuliwa watu pembezoni mwao?”[4]

وَأَن لَّوِ اسْتَقَامُوا عَلَى الطَّرِيقَةِ لَأَسْقَيْنَاهُم مَّاءً غَدَقًا

”Kama wangelinyooka kwenye njia, bila shaka Tungeliwanywesha maji kwa wingi.”[5]

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا

“Allaah amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi – kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao – na atawamakinishia dini yao aliyowaridhia na atawabadilishia amani badala ya khofu yao – [kwa sharti] wananiabudu Mimi na hawanishirikishi na chochote.”[6]

لِإِيلَافِ قُرَيْشٍ إِيلَافِهِمْ رِحْلَةَ الشِّتَاءِ وَالصَّيْفِ فَلْيَعْبُدُوا رَبَّ هَـٰذَا الْبَيْتِ الَّذِي أَطْعَمَهُم مِّن جُوعٍ وَآمَنَهُم مِّنْ خَوْفٍ

”Ili Quraysh wapate kuendelea na mazoea na amani walionayo, mazoea yao ya safari za majira ya baridi na majira ya joto. Hivyo basi wamwabudu Mola wa Nyumba hii, ambaye anawapa chakula kutokana na njaa na kuwapa amani kutokana na khofu.”[7]

Amani ni neema kubwa kabisa kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Sababu yake ni kushikamana na Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallm). Wakati nchi hii waliposhikamana na njia ilionyooka Allaah aliwapa uimara mzuri. Licha ya kwamba tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) awape matangamano wazuri, awalinde na matangamano wabaya ambao wanawapambia batili na awajaalie waweze kupupia kukaa na watu wazuri na wabora. Kwa hivyo tunapaswa kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kama ambavyo inawalazimu wananchi wa nchi hii nao kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kuna uwezekano ndani yake kuna watu waliojawa na matamanio ambao wanataka mambo yote kuhalalishwa na mengineyo. Allaah awajaze kheri watawala. Nimesoma katika gazeti namna ambavyo walimwomba mtawala Naayif (Hafidhwahu Allaah) kumfanya mwanamke naye awe mgombea. Akajibu:

“Mnataka mwanaume yeye ndiye abaki nyumbani na mwanamke ndiye atoke? Msijaribu kabisa.”

Wakamtaka akubali kuwepo kwa uchaguzi, lakini akajibu:

“Tumeona hayana mafanikio katika nchi za jirani. Hakika hakuna wanaoshinda isipokuwa tu watu wenye ushawishi na watu wenye pesa.”

Sahihi. Isitoshe ni jambo limetoka kwa maadui wa Uislamu.

Jumuiya ya haki za kibinaadamu imepokelewa na watu wengi licha ya batili nyingi iliyomo ndani yake. Kwa nini? Kwa sababu wanaona kuwa kutekeleza adhabu za Kishari´ah ni za kikatili na wanataka kufutilia mbali Qur-aan na Sunnah na kupenyeza sheria kutoka kwa maadui wa Uislamu. Serikali ya kisaudi – Allaah aiwafikishe juu ya kila kheri – wameipokea kwa sharti wawe ni wenye kunyenyekea Uislamu, Qur-aan na Sunnah na zile adhabu zilizowekwa katika Shari´ah. Mola wetu (´Azza wa Jall) anasema kuhusu kusimamisha adhabu zilizowekwa katika Shari´ah:

وَلَكُمْ فِي الْقِصَاصِ حَيَاةٌ

“Mtapata katika kisasi uhai.”[8]

Ni kweli kwamba mauaji na wizi ni kidogo katika nchi hii. Unaweza kuegesha gari yako karibu na msikiti au karibu na nyumba yako na hakuna anayekuja kuiiba. Katika baadhi ya miji mingine unaegesha gari na wakati unaporudi huioni. Bali wakati mwingine pengine wakaiba gari na dereva akiwa ndani yake. Hilo ni kutokana na sababu ya kutekeleza adhabu za Kishari´ah. Allaah awajaze kheri. Punde mmesikia maneno Yake Allaah (´Azza wa Jall):

وَلَكُمْ فِي الْقِصَاصِ حَيَاةٌ

“Mtapata katika kisasi uhai.”

Vivyo hivyo kuhusu mwizi. Atapojua kuwa utakatwa mkono wake basi atajizuia kuiba. Wakati mzinzi anapojua kuwa atapigwa bakoro ikiwa bado ni bikira au kupigwa mawe ikiwa ameshaingia katika ndoa, madhambi yatapungua. Sisemi kuwa hayatokuwepo, lakini yatapungua.

Miongoni mwa hayo ni kuwepo maafisa wa kidini wakiamrisha mema na kukemea maovu. Nimesoma katika gazeti ya kwamba mfalme Fahd (Hafidhwahu Allaah) amewapa maasifa wa kidini magari 300 na kuwaambia:

“Nyinyi ni kamati ya kuamrisha mema na sisi ni kamati ya udhibiti. Nyinyi mtaulizwa mbele ya Allaah.”

Allaah amjaze kheri.

Ameifanyia vyema nchi yake na wananchi wake. Ni wajibu kwa kila muislamu ulimwenguni kote kushirikiana na nchi hii ijapo ni kwa neno zuri. Wana maadui wengi ndani na nje ya nchi. Ndani ya nchi kuna watu wengi waliojawa matamanio wanaotaka kuhalalishwe kila kitu. Lakini Allaah amewakomesha kwa kuiimarisha nchi hii iliyobarikiwa. Kwa hivyo ni wajibu kwa kila muislamu kusaidiana na serikali hii.

Kisasi na adhabu za Kishari´ah ni neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) katika jamii. Wanatukosoa kwa kutekeleza adhabu moja wapo miongoni mwa adhabu za Allaah ilihali wao wenyewe wanawatokomeza watu! Visasi hivi vina manufaa kwa mtu mmojammoja na jamii nzima. Ni kifutio cha madhambi kwa mtu, kama ilivyopokelewa na al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh), na kulinda mali, damu na heshima ya jamii. Unaweza kutoka kwenda ufukweni au kokote pale na kumuona mtu na mke wake na hawana khofu juu ya yeyote. Adhabu hizi za Kishari´ah zina manufaa. Wakati zilipoondolewa katika nchi nyingi za Kiislamu ndipo wakashindwa kukabiliana na wezi, mambo ya jinai na utumiaji wa kileo na madawa ya kulevya. Yote haya ni kwa sababu ya kutotekeleza adhabu zilizowekwa katika Shari´ah.

Jengine ni kwamba nchi inajenga misikiti katika miji ya Kiislamu na nyenginezo. Hata hivyo tunawashauri wanapojenga misikiti wawakabidhi Ahl-us-Sunnah. Wakimpa msikiti Suufiy atawatukana. Atatoa Khutbah ijumaa kwa ajili ya kuwatukana. Wakimpa msikiti Hizbiy watautumia kwa ajili ya Hizbiyyah. Kwa hivyo nawashauri wawape misikiti Ahl-us-Sunnah ambao wanaipenda serikali hii na watawala wake.

Kuhusiana na jambo la uandishi, nimeulizwa nalo mara kadhaa. Yamo kwenye kanda. Nimewaamrisha ndugu ambao wanachapisha vitabu vyangu wasibakize kitu nilichoongea dhidi ya Saudi Arabia. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

هَلْ جَزَاءُ الْإِحْسَانِ إِلَّا الْإِحْسَانُ

”Je, kuna malipo ya wema isipokuwa wema?”[9]

Wametufanyia wema na kutukirimu kwa hali ya juu kabisa. Sisi sio miongoni mwa wale wanaokabili mazuri kwa mabaya. Hilo ni kutokana na fadhilah za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mimi nayasema haya. Hakuna yeyote aliyenisukuma kuyasema. Hakuna yeyote aliyenilazimisha kuyasema. Bali ni yenye kutoka kwangu. Naona kuwa nalazimika kuitakasa dhimma yangu.

[1] 5:66

[2] 7:96

[3] 28:57

[4] 29:67

[5] 72:16

[6] 24:55

[7] 106:1-4

[8] 2:179

[9] 55:60

  • Mhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Baraa-at-udh-Dhimmah
  • Imechapishwa: 14/04/2024