al-Lajnah ad-Daaimah kuhusu ujinga ni udhuru

Swali: Je, kila mwenye kufanya kitendo cha kufuru au shirki anakufuru? Pamoja na kwamba amefanya kitendo hichi kwa kutokujua. Je, anapewa udhuru kwa ujinga au hapewi? Je, ni zipi dalili juu ya kupewa udhuru au kutopewa udhuru?

Jibu: Ambaye ´ibaadah inamuwajibikia hapewi udhuru kwa kumuabudu asiyekuwa Allaah, kujikurubisha kwa kichinjwa kwa asiyekuwa Allaah, kuweka nadhiri kwa asiyekuwa Allaah na ´ibaadah nyenginezo kama hizo ambazo ni haki ya Allaah Pekee. Isipokuwa ikiwa kama atakuwa katika mji usiokuwa wa Kiislamu na hakufikiwa na Da´wah. Katika hali hii atapewa udhuru kwa kutofikiwa na si kwa ujinga tu. Muslim amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yake Muhammad iko Mikononi Mwake, hakuna yeyote katika Ummah huu atasikia kuhusu mimi, awe myahudi au mnaswara, kisha akafa na asiamini yale niliyotumwa nayo isipokuwa atakuwa ni katika watu wa Motoni.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumpa udhuru aliyemsikia. Anayeishi katika mji wa Kiislamu amesikia kuhusu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo hapewi udhuru katika misingi ya dini kutokana na ujinga wake.
Kuhusiana na wale waliomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awafanyie Dhaat Anwaat ili watundike silaha zao, watu hawa walikuwa ndio karibu wametoka katika ukafiri. Waliomba tu na hawakufanya. Walichokiomba ilikuwa ni kitu kinachoenda kinyume na Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwajibu kwa kitu chenye kutolea dalili ya kwamba lau wangelifanya walichokiomba basi wangelikufuru.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (2/33-34)
  • Imechapishwa: 24/08/2020