Pengine ni jambo munasibu kumnakilia msomaji yale yaliyoandikwa na mbebaji bendera wa leo ya Jahmiyyah na Mu´tazilah. Naye si mwengine ni yule anayeitwa Zaahid al-Kawthariy. Wanafunzi wanamjua al-Kawthariy na wanasikia kunazungumzwa juu yake.

al-Kawthariy alikuwa ni mwenye madhehebu ya ki-Hanafiy, mwenye ´Aqiydah ya Maaturiydiy ikiwa itaamuliwa. Lakini hata hivyo Allaah alimpa mtihani wa kuchukia Sunnah na Ahl-us-Sunnah na Muhaddithuun kutoka katika wale maimamu wakubwa mpaka hii leo. Hakuna imamu yeyote aliyeshikamana na Sunnah barabara ambaye amesalimika naye na khaswa Imaam ash-Shaafi´iy. Hakuna yeyote isipokuwa amemponda. Kila ambaye alimtambua kuwa anathibitisha sifa za Allaah na anawakemea wanafalsafa basi alikuwa adui yake. Pindi al-Kawthariy alipojua namna ambavyo Imaam as-Shaafi´iy amewazungumza wanafalsafa kwa njia ya kugonga kabisa pale aliposema:

“Ninaonelea kuwa mwanafalsafa anatakiwa kuchapwa kwa bakora na viatu. Azungushwe kati ya watu na kusemwe: “Haya ndio malipo kwa yule mwenye kuacha Qur-aan na Sunnah na akaenda katika falsafa.”

alichanganyikiwa. Ndipo akaanza kumshambulia imamu huyu. Wakati fulani anamtukana lugha yake. Wakati mwingine anamtukana ukoo wake. Waislamu wote, sembuse mwanafunzi, wanamjua ni nani Imaam ash-Shaafi´iy. Na kadhalika. Hakuna aliyesalimika naye isipokuwa tu yule ambaye alimtambua kuwa hawapondi wanafalsafa na falsafa. Vinginevyo hakuna yeyote katika Ahl-us-Sunnah ambaye alisalimika naye. Huyu ndiye al-Kawthariy kwa kifupi.

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad Amaan bin ´Aliy al-Jaamiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.sahab.net/forums/index.php?showtopic=139904
  • Imechapishwa: 08/01/2021