Ijulikane kuwa msingi wa kuweka nadhiri imechukizwa. Baadhi ya wanachuoni wamefikia mpaka kusema kuwa kimsingi ni haramu na haijuzu kwa mtu kuweka nadhiri. Mtu akiweka nadhiri ameikalifisha nafsi yake kwa jambo ambalo Allaah hakumkalifisha nalo. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amekataza mtu kuweka nadhiri na kusema:

“Nadhiri haiji kwa kheri. Hakika si vyenginevyo hukutokakwa mtu bakhili.”[1]

Lakini hata hivyo lau tutakadiria kuwa kuna mtu ameweka nadhiri, basi nadhiri imegawanyika sehemu mbali mbali:

1 – Nadhiri yenye hukumu ya kiapo.

2 – Nadhiri yenye ya maasi.

2 – Nadhiri ya utiifu.

1 – Kuhusiana na nadhiri yenye hukumu ya kiapo ni ile ambayo mtu amekusudia kukazia jambo; kukanusha au kuthibitisha, kusadikisha au kusisitiza. Kwa mfano mtu ameambiwa “wewe ulitwambia kadhaa na kadhaa lakini hukusema kweli.” Halafu akasema “ikiwa nimesema uongo basi Allaah ana nadhiri juu yangu ya kufunga mwaka mzima.” Hakuna shaka yoyote makusudio yake kwa kusema hivo ni kusisitiza maneno yake ili watu waweze kumsadikisha. Nadhiri aina hii ina hukumu ya yamini. Kwa sababu kwa kusema hivo amekusudia kusisitiza aliyoyasema. Mfano mwingine aseme “ikiwa sikufanya kadhaa, basi Allaah ana nadhiri juu yangu ya kufunga mwaka mzima.” Hapa pia amekusudia kusisitiza na kufanya aliyoyataja. Aina ya nadhiri kama hii ina hukumu ya kiapo. Dalili ya hili ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika si venginevyo kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kutokana na alichonuia.”[2]

Huyu amekusudia kiapo na atahukumiwa kwa alichonuia.

2 – Nadhiri ya haramu. Mtu akiweka nadhiri ya haramu haijuzu kwake kuitekeleza. Kwa mfano mtu aseme “Allaah ana nadhiri juu yangu ninywe pombe.” Hii ni nadhiri ya haramu. Si halali kwake kunywa pombe. Lakini kinyume chake kinachomuwajibikia ni kafara ya kiapo kutokana na maoni yaliyo na nguvu zaidi. Pamoja na kuwa kuna baadhi ya wanachuoni wanaonelea kuwa hana juu yake nadhiri kwa kuwa haikufungika. Lakini sahihi ni kwamba ameweka nadhiri na imefungika, lakini hata hivyo haijuzu kwake kuitekeleza. Mfano mwingine mwanamke aseme “Allaah ana nadhiri juu yangu nifunge siku zangu za hedhi.” Hili ni haramu. Haijuzu kwake kufunga siku zake za hedhi. Kinachomlazimu ni kafara ya kiapo.

3 – Nadhiri ya utiifu. Mtu aweke nadhiri ya utiifu. Kwa mfano aseme “Allaah ana nadhiri juu yangu kufunga masiku meupe: tarehe 13, 14 na 15.” Katika hali hii ni lazima kutimiza nadhiri yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuweka nadhiri ya kumtii Allaah, basi na amtii.”

Mfano mwingine aseme “Allaah ana nadhiri juu yangu nifunge rakaa mbili katika dhuhaa.” Ni lazima kutekeleza nadhiri yake kwa sababu ni utiifu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuweka nadhiri ya kumtii Allaah, basi na amtii.”

Nadhiri yake ikiwa ndani yake mna utiifu na yasiyokuwa utiifu, ni wajibu kutekeleza yale ambayo ni utiifu. Kuhusiana na yale ambayo sio utiifu asiyatekeleze na badala yake atoe kafara ya yamini. Ni kwa mfano wa kisa cha mtu huyu ambaye ameweka nadhiri ya kusimama kwenye jua na hatojikinga kivuli, hatozungumza na atafunga. Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuamrisha afunge kwa sababu ni utiifu. Ama kuhusu kusimama, kutojikinga na kivuli na kutozungumza, akamwamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akae kwenye kivuli, akae chini na azungumze.

[1]al-Bukhaariy (6693), (7792) na (6694) na Muslim (1639) na (1640).

[2]al-Bukhaariy (01) na Muslim (1907).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/238-239)
  • Imechapishwa: 22/09/2024