Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّـهُ مَرَضًا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ

“Ndani ya nyoyo zao yamo maradhi na Allaah akawazidishia maradhi na watapata adhabu iumizayo kwa waliyokuwa wakiyakadhibisha.”[1]

Makusudio ya maradhi hapa ni maradhi ya kuwa na shaka, utata na unafiki. Kwa sababu moyo hupatwa na maradhi aina mbili yanayoutoa kutoka katika uzima na kutengemaa kwake:

1- Maradhi ya shubuha za batili.

2- Maradhi ya matamanio mabaya.

Kufuru, unafiki, mashaka na Bid´ah yote haya ni katika maradhi ya shubuha.

Uzinzi, kupenda machafu na kufanya maasi ni katika maradhi ya matamanio. Amesema (Ta´ala):

فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ

“Akaja kutamani yule ambaye moyoni mwake mna maradhi.”[2]

Ni matamanio ya uzinzi. Msalimishwaji ni yule aliyesalimishwa kutokamana na maradhi haya mawili. Matokeo yake akawa na yakini na imani na subira kutokamana na kila maasi.

[1] 02:10

[2] 33:32

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, sid. 31
  • Imechapishwa: 07/05/2020