Umeandika kwenye barua yako:

“Nilipofika kwenye mlango wa tisa, nilikutana na kitu ambacho sikukitarajia kutoka kwa mtu kama wewe.”

  1. Je, waonelea kuwa nimemuasi Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwenda kinyume na Shari´ah ya Kiislamu pindi nilipobainisha haki? Si Allaah ndiye alichukua ahadi kutoka kwa watu wa Kitabu ya kubainisha haki na wasiifiche? Si ahadi hiyohiyo iliyochukuliwa kwetu? Si Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye aliomba kutoka kwa Maswahabah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati walipokuwa wanataka kumpa kiapo cha usikivu na utiifu katika Hadiyth ambayo imepokelewa na ´Ubaadah bin as-Saamitw:

“… na tuzungumze haki popote tulipo pasi na kuchelea lawama za mwenye kulaumu.”?

Allaah (´Azza wa Jalla) hakuwalaani wale wanaoficha haki wakati (Jalla wa ´Alaa) aliposema:

إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَى مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ أُولَئِكَ يَلعَنُهُمُ اللّهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ

“Hakika wale wanaoficha yale Tuliyoyateremsha katika hoja na uongofu baada ya kuwa tumeyabainisha kwa watu katika Kitabu, hao anawalaani Allaah na wanalaaniwa na kila mwenye kulaani.”?[1]

Si jambo la lazima kwa wanachuoni kuwaraddi wale wenye kwenda kinyume na Shari´ah na hukumu zake? Wakifanya mapungufu kwalo, basi wamefanya mapungufu katika wajibu uliofaradhishwa. Baadhi wakifanya hivo, haiwawajibikii wengine. Hata hivyo wanatakiwa kumuombea du´aa kwa kubainisha haki na kumshukuru baada ya kumshukuru Allaah badala ya kumtuhumu na kumjengea dhana mbaya.

Salaf siwalijisalimisha na jambo hili? Je, hawakutekeleza wajibu huu? Waliandika vitabu visivyohesabika kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah tokea wakati wa Taabi´uun mpaka hii leo na bado wanafanya hivo. Ee Shaykh! Si wewe ambaye uliandika vitabu viwili ukiwaraddi Ahl-ul-Bid´ah? Kitabu “Khabaar-ul-Aahaad” ambapo umewaraddi Mu´tazilah na wale wenye kuwafuata na kitabu “al-Faaiq fiy ar-Radd ´alaa man baddal al-Haqaaiq”. Naapa kwa Allaah ya kwamba nampenda mtu anayeitetea dini na kumraddi yule anayeingiza ndani kisichokuwemo.

Hata hivyo sijui ni kwa nini baadhi ya Mashaykh – Allaah awaongoze – wanapinda katika haki na kumkemea yule mwenye kutekeleza wajibu huu na kumzingatia kuwa ni mchokozi na mwenye kudhulumu. Lau mtu angelisema kitu cha ubinafsi juu yao, basi dunia nzima ingelisimama. Lakini wakati ambapo dini inatumiwa vibaya, haina neno! Je, namna hii ndivyo tumevoshikamana kiuadilifu na dini? Namna hii ndivyo tunavotekeleza wajibu wake? Au hii ni njia ya kuikandamiza dini na kupuuzia haki zake na kuacha mafundisho yake yakapotea hewani? Hili ni khaswa pale ambapo itakuwa inahusiana na misingi ya dini, kanuni zake na misingi yake inatumiwa vibaya na besi ya Tawhiyd inayovunjwa kwa shirki kubwa na Sunnah inayovunjwa kwa Bid´ah na haki inayovunjwa kwa batili. Unaonelea tunyamazie mambo kama hayo? Ninaapa kwa Allaah hatuwezi. Mmoja wenu ni lazima afanye faradhi hii. Mwenye kufanya hilo analipwa ujira na thawabu nyingi na Allaah.

[1] 02:159

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Radd-ul-Jawaab, uk. 13-15
  • Imechapishwa: 05/07/2020