Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ya pili ni maneno Yake (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Hivyo kwa sababu wao wamestahabu uhai wa dunia kuliko wa Aakhirah.” (16:107)

Kaweka wazi ya kwamba kukufuru huku na adhabu sio kwa sababu ya I´tiqaad, ujinga, kuichukia dini au kupenda kufuru, isipokuwa sababu yake ni kwa ajili ya kutaka kupata sehemu katika mambo ya dunia na kwa ajili hiyo akayapa kipaumbele mbele ya dini.

MAELEZO

Kukufuru kwa watu hawa ni kwa sababu ya kuyapa kipaumbele maisha haya ya dunia juu ya Aakhirah. Maisha haya kunamaanishwa kila chenye mafungamano na dunia kama kwa mfano wa cheo, mali, nafasi na uongozi. Yule ambaye anaipa kipaumbele dunia juu ya Aakhirah kutokana na yale yaliyomo ndani yake, anakuwa kafiri ijapokuwa atakuwa sio mwenye kupenda kufuru. Atakuwa ni mwenye kupenda zaidi dunia na kwa ajili hiyo anakufuru. Kuna watu ambao wanakufuru kwa sababu wanapenda ukafiri na unawapendeza. Wengine wanakufuru kwa sababu ya mali. Kuna wengine wanaokufuru kwa sababu ya nafasi. Wengine wanakufuru kwa sababu ya uongozi. Baadhi wanakufuru ili waweze kufikia kitu katika utawala. Kuna sababu nyingi.

Tunamuomba Allaah (Ta´ala) atuhidi katika njia iliyonyooka na asizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 104-105
  • Imechapishwa: 02/12/2023