Kuhusu mahali inapotolewa Zakaat-ul-Fitwr ataitoa kuwapa mafukara wa maeneo alipo wakati wa kutolewa kwake. Ni mamoja mtu huyo anaishi maeneo hayo au haishi maeneo hapo muda wa kuwa ni katika miji ya waislamu na khaswa ikiwa ni maeneo penye ubora kama vile Makkah na Madiynah au mji ambao mafukara wake wana haja kubwa zaidi. Ikiwa ni katika nchi ambayo hakuna wa kuwapa nayo au hajui ambao wanaiistahiki, basi atawakilisha mtu ambaye atawapa nayo wale ambao wanaiistahiki.

Watu ambao wanastahiki kupewa Zakaat-ul-Fitwr ni wale mafukara. Na wale ambao wana madeni ambayo wameshindwa kuyalipa watapewa sehemu katika zakaah kwa kiasi cha haja.

Inafaa kumpa Zakaat-ul-Fitwr zaidi ya fukara mmoja. Inafaa chakula cha masikini kadhaa kumpa masikini mmoja. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikisia wajibu na wala hakukadiria nani anayepewa nayo. Kutokana na hilo iwapo mtu atakusanya vyakula vya watu wengi ndani ya chombo kimoja baada ya kupimwa kiwango chake na baada ya hapo akawa anakigawa chakula hicho bila ya kukipima tena itasihi. Lakini anapaswa kumjuza yule fakiri kwamba hawajui ni kiasi gani walichompa ili asije kudanganyika na matokeo yake akajitolea yeye mwenyewe ilihali hajui kipimo chake.

Inafaa kwa fakiri baada ya kupokea chakula kutoka kwa mtu akajitolea nacho mwenyewe au akamtolea mmoja katika familia yake iwapo atakipima chakula hicho au mtoaji akamweleza kuwa kimekamilika na yeye akawa anaamini maneno yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 212-213
  • Imechapishwa: 26/03/2024