Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

78 – Kuzama na kupekua jambo hilo kutampelekea katika kukoseshwa nusura, kunyimwa na kuchupa mipaka.

79 – Kwa hivyo jihadhari kwelikweli kuipekua, kufikiri na kuwa na wasiwasi juu ya jambo hilo. Kwani Allaah (Ta´ala) amewaficha ujuzi wa makadirio viumbe Wake na akawakataza kujitahidi kuijua.

MAELEZO

Haya ni maneno matukufu. Kuingia ndani zaidi katika mambo ya makadirio na kushughulisha wakati, nafsi na moyo kunapelekea katika mashaka na mtu kuacha kufanya matendo. Mambo hayo hayana maana na ni kunyimwa nusura. Wakati Allaah anamkoseshwa nusura mja basi humshughulisha na mambo hayo, na pindi Allaah anapomkirimu mja basi humshughulisha na kumtii na akatumia vizuri wakati wake. Tuna mipaka ambayo hatutakiwi kuivuka. Allaah hajatuwajibishia kupekua mipango na makadirio; lakini ametuwajibishia kuamini mambo hayo kwa sisi kutenda matendo mema na kujiepusha na matendo mabaya.

Tahadharini na mambo hayo. Tahadharini kupekua mada hiyo. Tahadharini na kuifikiri. Wasiwasi ni kusitasita na kuwa na mashaka. Achana na mambo yote hayo na ufunge kabisa mlango huo. Huku ni kutilia mkazo yale yaliyokwishatangulia kwamba makadirio ni siri ya Allaah (Ta´ala). Allaah (Ta´ala) amewaficha viumbe Wake ujuzi huo kwa sababu ni kitu ambacho hakina faida yoyote na wao. Amewakataza kujitahidi kuyajua mambo ya makadirio. ´Amr bin Shu´ayb amesimulia kutoka kwa baba yake ambaye na yeye amepokea kutoka kwa baba yake (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

”Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatokea Maswahabah zake ambao walikuwa wakigombana juu ya makadirio. Akageuka mwekundu usoni kana kwamba ni komamanga kutokana na kughadhibika na akasema: ”Je, mmeumbwa kwa ajili ya jambo hilo? Mnataka kugonganisha Qur-aan kwa Qur-aan? Hayo ndio yaliyowafanya nyumati kabla yenu kuangamia.”[1]

[1] Ibn Maajah (85). Nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah”.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 112-113
  • Imechapishwa: 30/10/2024