97. Hakuna anayepewa udhuru kwa kukufuru isipokuwa yule mwenye kulazimishwa

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Aayah ya pili ni maneno Yake (Ta´ala):

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya imani yake [atapata adhabu] isipokuwa yule aliyekirihishwa na huku moyo wake umetua juu ya imani. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu. Hivyo kwa sababu wao wamestahabu uhai wa dunia kuliko wa Aakhirah.” (16:106)

Allaah hakumpa udhuru yeyote katika watu hawa, isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake umetua juu ya imani. Ama mbali na mtu huyu, amekufuru baada ya kuamini kwake, ni mamoja ikiwa kafanya hilo kwa khofu, kwa kujikombakomba au kutaka cheo, watu wake, familia yake au mali, au kafanya hilo kwa mzaha au sababu zingine miongoni mwa sababu – isipokuwa aliyelazimishwa tu.

MAELEZO

Hii ndio Aayah ya pili ambayo mtunzi (Rahimahu Allaah) anataka mtu aizingatie. Aayah hii inajulisha kuwa hakuna yeyote anayepewa udhuru kukufuru baada ya kuamini kwake isipokuwa yule mwenye kutenzwa nguvu. Mwenye kukufuru kwa khiyari yake mwenyewe kutokana na sababu yoyote ile – pasi na kujali ni kwa sababu ya mzaha, mapenzi ya kupenda kazi, kutetea nchi yake na mfano wa hayo – anazingatiwa kuwa ni kafiri. Allaah (´Azza wa Jall) hatompa udhuru yeyote mwenye kukufuru, isipokuwa tu yule mwenye kufanya hivo kwa kulazimishwa na kwa sharti wakati huohuo moyo wake uwe umetua juu ya imani.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 103-104
  • Imechapishwa: 28/11/2023