95. Ulazima wa kulichimba kaburi chini zaidi, kuwa pana na uzuri

93- Ni lazima kuifanya kaburi kwenda chini sana, kuipanua na kuifanya uzuri. Kumepokelewa Hadiyth mbili juu ya hilo:

Ya kwanza: Hishaam bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Ilipokuwa siku ya Uhud waliuliwa walioluwa katika waislamu na baadhi ya wengine wakapatwa na majeraha. [Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Kumchimbia kila mmoja shimo lake ni jambo gumu], [unatuamrisha tufanye nini]. Akasema: “Chimbeni, fanyeni upana na [fanyeni kina] [na fanyeni uzuri] na wazikeni wawiliwawili na watatuwatatu ndani ya kaburi moja na mumtangulizeni yule ambaye ni mwingi wao wa Qur-aan. [Baba yangu akawa ndiye wa tatu katika wale watatu na yeye akawa ndiye mwingi wao wa Qur-aan. Hivyo akatangulizwa mbele].”

Ameipokea Abu Daawuud (02/70), an-Nasaa´iy (01/273-274), at-Tirmidhiy (03/36), al-Bayhaqiy (04/34), Ahmad (04/19, 20) na Ibn Maajah kwa mukhtasari.

Mtiririko ni wa an-Nasaa´iy na ziada zote ni zake katika upokezi. Vivyo ndivo imepokelewa kwa Ahmad pasi na ya kwanza. Abu Daawuud na al-Bayhaqiy wanayo ziada ya tatu. at-Tirmidhiy, Ibn Maajah na al-Bayhaqiy wanayo ziada ya nne. at-Tirmidhiy anayo ziada ya tano na amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Cheni ya wapokezi wake ni yenye kuzuguka kwa Humayd bin Hilaal. Ayyuub as-Sikhtiyaaniy amepokea kutoka kwake kwa njia tatu:

1- Kutoka kwake kutoka kwa Hishaam bin ´Aamir.

2- Kutoka kwake Abud-Dahmaa´ kutoka kwa Hishaam.

3- Kutoka kwa Sa´d bin Hishaam kutoka kwa baba yake Hishaam.

Sulaymaan bin al-Mughiyrah wamemfuata katika njia ya kwanza kutoka kwa Humayd kutoka kwake.

Ameipokea an-Nasaa´iy na al-Bayhaqiy (03/413) na Ahmad.

Jariyr bin Haazim amemfuata katika njia ya tatu: Humayd bin Hilaal ametuhadithia, kutoka kwa Sa´d bin Hishaam bin ´Aamir.

Wameipokea watatu waliotajwa na kadhalika Abu Daawuud na al-Bayhaqiy (03/414) kutoka kwake. Njia hii ndio yenye nguvu zaidi kwangu kwa ajili ya ufuatiliaji huu. Ndio yenye nguvu zaidi kuliko ule ufuatiliaji wa kwanza kwa njia mbili:

1- Muslim amemjengea hoja Sulaymaan bin al-Mughiyrah pasi na al-Bukhaariy. Amemsimulia hali ya kumwambatanisha na mwengine kinyume na Jariyr bin Haazim ambaye ametumiwa kama hoja na Muslim na al-Bukhaariy.

2- Ndani yake kuna ziada kutoka kwa mtu ambaye ni mwaminifu na ni yenye kuzingatiwa. Hivyo ikawa ni yenye nguvu.

Kutokana na haya cheni ya wapokezi ya Hadiyth ni Swahiyh, kama alivosema at-Tirmidhiy. Nayo iko kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.

Ya pili: Kutoka kwa bwana mmoja katika Answaar:

“Tulitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mazishi ya bwana mmoja katika Answaar. Kipindi hicho mimi nilikuwa kijana pamoja na baba yangu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya ukinga wa lile kaburi. Akawa anausia [Katika upokezi mwingine imekuja: “Akimwashiria] mchimbaji na akisema: “Lipanue upande wa kichwa, lipanue upande wa miguu. Huenda kaburi hili likawa ni neema miongoni mwa neema za Peponi.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/83), al-Bayhaqiy (03/414) na upokezi mwingine ni wake, Ahamd (05/408) na mtiririko ni wake. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Hivo ndivo alivosema an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (05/286) na al-Haafidhw katika “at-Talkhiysw” (05/201).

Udhahiri wa amri katika Hadiyth ni kwamba unaonyesha kuwa ni lazima kutokana na yale yaliyotajwa ndani yake katika ukina, upana na ufanyaji vizuri. Kinachotambulika kutoka kwa Shaafi´iyyah na wengineo ni mapendekezo ya kwenda chini zaidi. Ama kuhusu Ibn Hazm amesema ulazima kwa uwazi katika “al-Muhallaa” (05/116).

Wametofautiana juu ya ukomo wa ukina kwa maoni mbalimbali ambayo unaweza kuyaona katika “al-Majmuu´” au kwenginepo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 181-182
  • Imechapishwa: 21/02/2022