95. Mfano wa vitu ambavo havisihi kutolewa kama Zakaat-ul-Fitwr

Kwa msemo mwingine haisihi mtu akaoa Zakaat-ul-Fitwr kuwapa wanyama kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameifaradhisha kuwapa chakula masikini na sio kuwapa wanyama.

Wala haisihi kutoa Zakaat-ul-Fitwr vitu kama nguo, matandiko, vyombo, mizigo na vyenginevyo visivyokuwa vyakula vinavyoliwa na watu. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefaradhisha kuwa ni chakula. Kwa hiyo mtu asivuke kile alichokilengesha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Wala haisihi kutoa thamani ya chakula, kwa sababu kufanya hivo ni kwenda kinyume na yale aliyoamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imethibiti kutoka kwake ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

Ameipokea Muslim.

Isitoshe kutoa kima cha pesa ni kwenda kinyume na matendo ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum), kwani wao walikuwa wakitoa pishi ya chakula. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jilazimiane na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na walioongozwa baada yangu.”[1]

Jengine ni kwamba Zakaat-ul-Fitwr ni ´ibaadah iliyofaradhishwa kutokana na aina maalum. Kwa hivyo haisihi kutoa kile ambacho sio katika aina hiyo maalum kama ambavo haisihi kuitoa kinyume na wakati wake maalum.

Aidha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amiefanya kuwa maalum kutokana na aina mbalimbali. Hivyo basi, ingelikuwa kima cha pesa ni chenye kuzingatiwa kuwa ingelipasa aina ya pishi na yale yanayolingana na thamani yake katika aina mbalimbali.

Isitoshe ni kwamba kutoa kima cha pesa kunafanya kule kutoa chakula kutoka nje ya nembo yenye kuonekana waziwazi na kwenda katika swadaqah yenye kujificha. Kutoa pishi ya chakula kunafanya ni nembo yenye kudhihiri kati ya waislamu na yenye kutambulika kwa mdogo na kwa mkubwa ambao wote watashuhudia kupimwa kwake na kugawanywa kwake na itatambulika baina yao. Hilo ni tofauti na pale ambapo mtu anatoa pesa kwa siri baina yake na huyo mpewaji.

[1] Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Maajah na at-Tirmidhiy ambaye amesema:

”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Abu Nu´aym amesema:

”Hadiyth ni nzuri sana katika Hadiyth Swahiyh za watu wa Shaam.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 209-210
  • Imechapishwa: 21/03/2024