95. Hakuna imamu yeyote aliyesema kuwa Allaah yuko kila mahali

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Hajapatapo yeyote katika wao siku hata moja kusema kwamba Allaah hayuko juu ya mbingu.

Hajapatapo yeyote katika wao siku hata moja kusema kwamba Allaah hayuko juu ya ´Arshi.

Hajapatapo yeyote katika wao siku hata moja kusema kwamba Allaah yuko kila mahali.

Hajapatapo yeyote katika wao siku hata moja kusema kwamba mahali pote kwa Allaah ni zenye kulingana.

MAELEZO

Hakuna yeyote katika wale maimamu wanaozingatiwa ambaye amekanusha kuwepo kwa Allaah juu ya viumbe au kulingana Kwake juu ya ´Arshi. Bali vitabu vyao wote vinathibitisha juu ya kuthibitisha jambo hilo.

Hajapatapo yeyote katika wao siku hata moja kusema kama wanavosema Huluuliyyah, ya kwamba yuko kila mahali. Hawamtakasi hata kutokana na maeneo ya taka, vyoo na maeneo machafu – Allaah ametakasika kutokana na yale wanayoyasema! Bali baadhi yao wanaenda mbali mno na kufikia kusema kuwa amekita ndani ya viumbe. Huluuliyyah hawatofautishi kati ya bahari na ´Arshi – vyote vinalingana. ´Arshi haikhusishwi kwa chochote – vyote ni viumbe, hakuna chochote ambacho kina sifa ya kipekee. Aidha wanadai kuwa Allaah yuko kila mahali; yuko juu ya mbingu, juu ya ´Arshi, juu ya bahari, ardhini na kila mahali – Allaah ametakasika kutokana na yale wanayoyasema! Haki ni kwamba Yuko juu ya ´Arshi, juu ya mbingu. Ujuzi Wake umeenea kila mahali. Amesema (Ta´ala):

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

“Yeye Ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ‘Arshi. Anajua yale yanayoingia ardhini na yale yatokayo humo na yale yanayoteremka kutoka mbinguni na yale yanayopanda humo – Naye yupamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah ni Mwenye kuona yote myafanyayo.”[1]

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَخْفَىٰ عَلَيْهِ شَيْءٌ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ

“Hakika Allaah hakifichiki Kwake chochote katika ardhi wala katika mbingu.”[2]

[1] 57:4

[2] 03:05

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 137-138
  • Imechapishwa: 01/09/2024