Wakati fulani[1] alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) analeta Qunuut katika Rak´ah ya mwisho ya Witr[2]. Ilikuwa inaweza kutokea anasoma Qunuut kabla ya kwenda katika Rukuu´[3].

Alimfunza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) al-Hasan bin ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kusema [pindi anapomaliza kisomo katika Witr]:

اللهم اهدِنا فيمَن هديت وعافنا فيمن عافيت وتولنا فيمن توليت وبارك لنا فيما أعطيت وقِنا شر ما قضيت [ف]انك تقضي ولا يقضى عليك [و]اٍنه لا يذل مَن واليت [ولا يعزُ من عاديت]تباركت ربنا وتعاليت لا منجا منك إلا إليك

“Ee Allaah! Niongoze pamoja na Uliowaongoza, nisalimishe pamoja na Uliowasalimisha na nilinde pamoja na Uliowalinda. Tubariki katika kile Ulichotupa na tukinge na shari ya Uliyotuhukumia. Kwani hakika Wewe unahukumu wala huhukumiwi. Hakika hadhaliliki Uliyemlinda, na wala hatukuki Uliyemfanya adui[4]. Umebarikika, ee Mola wetu, na umetukuka. Hakuna mahali pa kuokoka kwengine isipokuwa Kwako.”[5]

[1] Nimesema wakati fulani kwa sababu Maswahabah waliopokea Witr wamefanya hivo pasi na kutaja Qunuut. Lau Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angelikuwa na mazowea hayo basi wote wangelipokea kutoka kwake. Kwa vile Ubayy bin Ka´b pekee ndiye kapokea kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi hiyo ina maana kwamba alisoma Qunuut nyakati fulani peke yake.  Ni dalili inayoonyesha kuwa Qunuut sio wajibu. Haya ndio maoni ya wanachuoni wengi. Kwa hiyo mhakiki Ibn-ul-Hammaam mwenyewe amekubali katika ”Fath-ul-Qadiyr” (1/306 na 359-360) kwamba maoni yanayowajibisha Qunuut ni dhaifu na yasiyokuwa na dalili. Ni dalili ya uadilifu wake na kutokuwa na ushabiki. Maoni aliyofikia yanapingana na madhehebu yake.

[2] Ibn Nasr na ad-Daaraqutwniy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh

[3] Ibn Abiy Shaybah (1/41/12), Abu Daawuud, an-Nasaa’iy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (2-1-218), Ahmad, at-Twabaraaniy, al-Bayhaqiy na Ibn ´Asaakir (2/244/4) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Kupitia kwake Ibn Mandah katika “at-Tawhiyd” (02/70) amepokea du´aa peke yake. Imepokelewa kwa cheni ya wapokezi nyingine ilio nzuri. Nimeitaja katika “al-Irwaa´” (426).

an-Nasaa´iy amepokea ziada mwishoni mwa Qunuut:

و صل الله على النبي الأمي

“na Allaah amsifu Mtume ambaye si msomi.”

Cheni ya wapokezi wake ni dhaifu kwa mujibu wa Haafidhw Ibn Hajar, al-Qastwalaaniy, az-Zarwaaniy na wengineo. Ndio maana sikutaja nyongeza hiyo kwa sababu haikutimiza masharti niliyoyaweka kwenye utangulizi wa kitabu. al-´Izz bin ´Abdis-Salaam amesema:

“Haikusihi kupokelewa kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asifiwe katika Qunuut. Kwa ajili hiyo kusiongezwe kusifiwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” (al-Fataawaa (1/66))

Hapa anaonyesha kwamba hakupanua mipaka ya maoni yanayosema juu ya Bid´ah nzuri, kama walivyofanya baadhi ya wale waliokuja nyuma.

Hata hivyo nimejirekebisha na kusema kwamba imethibiti kuwa Ubayy bin Ka´b (Radhiya Allaahu ´anh) alimsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwishoni mwa Qunuut wakati alipoongoza swalah wakati wa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh). Yamepokelewa na Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” (1097). Kadhalika yamethibiti kutoka kwa Abu Haliymah Mu´aadh al-Answaariy ambaye aliongoza swalah katika wakati huo. Yamepokelewa na al-Qaadhwiy Ismaa´iyl (107) na wengineo. Kwa hivyo ni Shari´ah nyongeza kwa sababu imetendewa kazi na Salaf. Kwa ajili hiyo haifai kusema kwamba ni Bid´ah na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[4] Nyongeza hii imethibiti katika Hadiyth, kama alivosema Haafidhw Ibn Hajar katika “at-Talkhiysw”. Hayo nimeyafikia katika asili. Hayo yamempita an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) katika ”Rawdhat-ut-Twaabiyn” (1/253) na akasema kuwa ni nyongeza ya wanachuoni kama ambavo walizidisha:

فلك الحمد على ما قضيت، أستغفرك وأتوب إليك

“Ni Mwenye kuhimidiwa kwa yale Uliyohukumu na nakuomba msamaha na natubia Kwako.”

Lililo la ajabu ni kwamba punde tu baada ya baadhi ya misitari akasema:

“Wamekubaliana juu ya kosa la al-Qaadhwiy Abut-Twayyib pindi alipokataa jumla “Wala hatukuki Uliyemfanya adui”. Imepokelewa katika upokezi wa al-Bayhaqiy na Allaah ndiye anajua zaidi.”

[5] Ibn Khuzaymah (2/119/1), Ibn Abiy Shaybah na wale waliotajwa pamoja naye katika marejeo yaliyotangulia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 156-157
  • Imechapishwa: 08/01/2019