94. Je, kuna uwezekano wa kukusanyika na makundi na mapote mengine?

Swali 94: Je, kuna uwezekano wa kuwa na umoja licha ya makundi mengi? Ni mfumo upi ambao ni lazima kukusanyika juu yake?

Jibu: Haiwezekani kukusanyika licha ya makundi mengi. Kwa sababu makundi yako kinyume haya kwa yale. Haiwezekani kukusanya kati ya vinyume viwili. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane!”[1]

Amekataza (Subhaanah) kufarikiana na akaamrisha kukusanyika juu ya kundi limoja – nalo ni kundi la Allaah:

أُولَـٰئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ ۖ وَيُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ رَضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ اللَّـهِ ۚ أَلَا إِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

”Hao [Allaah] amewaandikia katika nyoyo zao imani na akawatia nguvu kwa Roho kutoka Kwake na atawaingiza kwenye mabustani yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Allaah ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hao ndio kundi la Allaah. Tanabahi! Hakika kundi la Allaah ndio lenye kufaulu.”[2]

وَإِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ

”Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja Nami ni Mola wenu. Hivyo nicheni.”[3]

Mapote na makundi yanayotofautiana hayana chochote kuhusiana na Uislamu. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

“Hakika wale waliofarikisha dini yao na wakawa makundi makundi huna lolote kuhusiana na wao. Hakika amri yao iko kwa Allaah, kisha atawajulisha kwa yale waliyokuwa wakifanya.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mayahudi wamegawanyika makundi sabini na moja. Manaswara wamegawanyika makundi sabini na mbili.  Na Ummah wangu utagawanyika katika mapote sabini na mbili. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: ”Ni lipi hilo, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Ni lile linalofuata yale ninayofuata mii hii leo na Maswahabah zangu.”[5]

Hakuna kundi lililookoka isipokuwa tu moja na mfumo wake ni yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Mengine yote ni yanatenganisha na hayakusanyi. Amesema (Ta´ala):

وَّإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا هُمْ فِي شِقَاقٍ

“Wakikengeuka [na kwenda njia nyingine], basi hakika wao wamo katika upinzani.”[6]

Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

”Hautotengemaa mwisho wa ummah huu isipokuwa kwa yale yaliyowafanya wa mwanzo wao kutengemaa.”[7]

Amesema (Ta´ala):

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[8]

Hatukusanyiki isipokuwa juu ya mfumo wa Salaf peke yake.

[1] 3:103

[2] 58:22

[3] 23:52

[4] 06:159

[5] Ibn Maajah (3992), at-Tirmidhiy (2641) na Abu Daawuud (4596). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Mishkaat-ul-Maswaabiyh” (171).

[6] 2:137

[7] Tazama ”at-Tamhiyd” (10/23) ya Ibn ´Abdil-Barr.

[8] 09:100

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 225-227
  • Imechapishwa: 06/08/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy