Allaah amekuwekeeni katika kumalizia mwezi wenu huu utoaji wa Zakaat-ul-Fitwr kabla ya kuswaliwa swalah ya ´iyd. Katika kikao hichi tutazungumzia hukumu yake, hekima yake, kiwango chake, wakati wa kuwajibika kwake, utolewaji wake na mahali pake.

Kuhusu hukumu yake ni faradhi ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewafaradhishia waislamu. Yale aliyofaradhisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yana hukumu sawa na yale aliyofaradhisha Allaah (Ta´ala) au yale aliyoamrisha. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖ وَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا

“Atakayemtii Mtume basi huyo amemtii Allaah; na atakayempa mgongo basi [atambue] hatukukutuma kuwa mlinzi juu yao.”[1]

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

”Yule atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na ni uovu ulioje mahali pa kuishia!”[2]

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.”[3]

Ni faradhi kwa mkubwa, mdogo, mvulana, msichana, muungwana na mtumwa katika waislamu. ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifaradhisha kutoa pishi ya tende au pishi ya shayiri kuwa ni Zakaat-ul-Fitwr iliyowajibika kwa waislamu wote; mtumwa na aliye huru, mwanamume, mwanamke, mtoto mdogo na mzee na kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Sio wajibu kwa mimba ya mtoto aliyeko tumboni isipokuwa ikiwa kama mtu atajitolea kufanya hivo hapana vibaya. Kiongozi wa waumini, ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akimtolea mimba ya mtoto aliyeko tumboni.

Mtu analazimika kujitolea mwenyewe na wale ambao analazimika kuwahudumia kukiwemo mke au jamaa wengine ikiwa hawawezi kujitolea wao wenyewe. Wakiweza kujitolea wenyewe basi ndio bora kwa sababu msingi wao ndio wanazungumzishwa. Zakaat-ul-Fitwr haiwi wajibu isipokuwa kwa kile kilichozidi yale matumizi yake ya mchana wa ´iyd na usiku wake. Asipopata isipokuwa chini ya pishi moja tu ataitoa. Amesema (Ta´ala):

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninapokuamrisheni jambo, basi lifanyeni muwezavyo.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

[1] 04:80

[2] 04:115

[3] 59:07

[4] 64:16

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 207-208
  • Imechapishwa: 19/03/2024