93. Athar ”Sunnah wakati wa swalah ya jeneza ni kusoma… ”

94 – Muhammad bin al-Muthannaa ametuhadithia: ´Abdul-A´laa ametuhadithia: Ma´mar ametuhadithia, kutoka kwa az-Zuhriy: Nimemsikia Abu Umaamah Sahl bin Haniyf akisimulia kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyab, ambaye amesema:

”Sunnah wakati wa swalah ya jeneza ni kusoma ”al-Faatihah”, kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kisha kumtakasia du´aa yule maiti wakati mtu anapomaliza. Mtu asiisome isipokuwa mara moja tu. Halafu alete Tasliym.”[1]

[1] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Abu Umaamah alikuwa Swahabah mdogo, kama alivosema Ibn-ul-Qayyim katika “Jalaa’-ul-Afhaam”, uk. 253. Ameyapokea haya kutoka kwa jopo la Maswahabah. Yuunus amesimulia kutoka kwa Ibn Shihaab: Abu Umaamah bin Sahl bin Haniyf amenikhabarisha, ambaye alikuwa miongoni mwa wakubwa na wanazuoni wa Wanusuraji na alikuwa mmoja katika wale watoto walioshiriki vita vya Badr pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ameeleza kuwa wanamme wengi katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamemuhadithia:

”Katika swalah ya jeneza imamu anatakiwa kuleta Takbiyr, kisha amswalie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… ”

az-Zuhriy amesema:

”Ametuhadithia hayo Abu Umaamah na huku Sa´iyd al-Musayyab akisikiza, na hakumpinga jambo hilo.”

Ibn Shihaab amesema:

”Nikamtajia Muhammad bin Suwayd aliyonieleza Abu Umaamah juu ya kumswalia maiti, akasema: ” ”Na mimi nimemsikia adh-Dhwahhaak bin Qays akihadithia kutoka kwa Habiyb bin Maslamah, ambaye aliswali swalah ya jeneza vivyo hivyo kama alivyotuhadithia Abu Umaamah.”

Tazama “Ahkaam-ul-Janaa-iz”. Hadiyth hiyo ameipokea al-Haakim, kupitia kwake, al-Bayhaqiy. al-Haakim amesema:

”Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye, mambo ni kama alivosema. an-Nasaa´iy pia ameipokea kupitia kwa al-Layth, kutoka kwa Ibn Shihaab kwa mukhtaswari.

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Ishaaq al-Maalikiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-us-Swalaah ´alaan-Nabiy, uk. 80-81
  • Imechapishwa: 13/02/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy