Allaah amewaficha usiku wa makadirio waja Wake kwa sababu ya kuwaonea huruma ili matendo yao yawe mengi wakati wa kuutafuta katika nyusiku hizo tukufu kukiwemo kuswali, kufanya Dhikr na kuomba du´aa. Hivyo wawe karibu zaidi na Allaah na thawabu nyingi. Jengine ni kwamba amewaficha nao ili abainike ambaye ni mkweli na mwenye kuupupia katika kuutafuta kutokana na ambaye ni mvivu na mzembe. Hakika ambaye anapupia jambo basi anafanya bidii katika kulitafuta na yale masumbuko yanayomkumba yanamkuwia mepesi wakati wa kufikia malengo yake.

Wakati mwingine Allaah huwaonyesha baadhi ya waja Wake alama na ishara yake. Ni kama ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona alama yake kwamba asubuhi yake anasujudu katika maji na matope. Ndipo usiku huo kukanyesha mvua na akasujudu katika swalah ya Subh kwenye maji na matope.

Ndugu zangu! Mlango unafunguliwa katika usiku wa makadirio, wapenzi hujikurubisha, yanasikizwa maombi mbalimbali na yanaitikiwa. Wanaofanya matendo wanaandikiwa malipo makubwa. Usiku wa makadirio ni bora kuliko miezi elfu. Kwa hivyo jitahidini – Allaah akurehemuni – kuutafuta. Huu ndio wakati wa kuutafuta. Tahadharini na kughafilika, kwani katika kughafilika kuna maharibiko.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 163-164
  • Imechapishwa: 18/03/2024