Bid´ah zote katika dini ni haramu na upotevu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nakutahadharisheni na mambo ya kuzua. Hakika kila kitachozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

“Atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”[2]

 Katika upokezi mwingine:

“Mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”[3]

Hadiyth mbili zimefahamisha kwamba kila kitachozuliwa katika dini ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu na ni yenye kurudishwa nyuma. Maana ya hayo ni kwamba uzushi katika ´ibaadah na mambo ya imani ni haramu. Lakini uharamu unatofautiana kutegemea na aina yenyewe ya Bid´ah hiyo.

Kuna ambazo ni ukafiri wa wazi kabisa. Kama mfano wa kuyatufu makaburi kwa ajili ya kujikurubisha kwa mwenye nayo, kuyatangulizia vichinjwa na nadhiri, kuwaomba wenye nayo, kuwataka msaada na vilevile maneno ya wale Jahmiyyah na Mu´tazilah waliopindukia.

Bid´ah nyenginezo ni njia zinazopelekea katika shirki. Kama mfano wa kujenga juu ya makaburi, kuswali na kuomba du´aa kwenye makaburi hayo.

Bid´ah nyenginezo ni ufuska wa kiimani. Kama mfano wa Bid´ah za Khawaarij, Qadariyyah na Murji-ah katika maneno na imani zao zinazokwenda kinyume na dalili za Kishari´ah.

Bid´ah nyenginezo ni maasi kama mfano wa Bid´ah za kutotaka kuoa, kufunga hali ya kuwa mtu ameshinda anasimama juani, kujishughulisha na ´ibaadah kwa lengo la kutaka shahawa za jimaa[4].

[1] Ahmad (17184), Abu Daawuud (4607) na tamko ni lake, at-Tirmidhiy (2681) na Ibn Maajah (42).

[2] al-Bukhaariy (2550) na Muslim (1718).

[3] Muslim (4468).

[4] al-I´tiswaam (02/37) ya ash-Shaatwibiy.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 180-181
  • Imechapishwa: 30/06/2020