Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya swawm ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu – ili mumche.”[1]

MAELEZO

Swawm si lazima isipokuwa kwa waislamu. Kuhusu makafiri haisihi kutoka kwao mpaka washuhudie kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad (Swalla Allahau ´alayhi wa sallam) ni  Mtume wa Allaah. Muda wa kuwa wamo juu ya ukafiri haitowafaa kitu ´ibaadah si swawm wala ´ibaadah nyingine. Kwa ajili hiyo ndio maana amewazungumzisha waumini peke yao kwa sababu wao ndio wenye kuitikia. Wao ndio ambao swawm inasihi kutoka kwao na ndio ambao swawm inakubaliwa kutoka kwao.

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَام

“Mmefaradhishiwa swawm… “

Mmeandikiwa maana yake mmefaradhishiwa. Ni kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ

”Mmefaradhishiwa kupigana vita.”[2]

Bi maana mmefaradhishiwa kupigana. Kuandikiwa ndani ya Qur-aan maana yake ni kufaradhishiwa:

كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ

“… swawm kama ilivyoandikwa kwa walio kabla yenu.”

Kama ilivyofaradhishwa kwa nyumati zilizokuwa kabla yenu. Ni dalili inayofahamisha kuwa swawm ilikuwa yenye kutambulika kwa nyumati zilizotangulia na katika Shari´ah zilizotangulia. Si jambo maalum juu ya Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuna uwezekano kwa nafsi ikalemewa na swawm kutokana na kujizuia kutokamana na matamanio. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amebainisha kuwa ameisunisha juu ya viumbe Wake na kwamba ni kwa nyumati zote. Hata kabla ya kuja Uislamu swawm ilikuwa yenye kutambulika. Walikuwa wakifunga siku ya ´Aashuuraa´.

لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“”… ili mumche.”

Hapa kunabainishwa hekima ya kufunga. Kumebainishwa hekima ya kuwekwa kwa funga. Hekima yenyewe ni kwamba inasababisha kumcha Allaah. Kwa sababu wakati wa kufunga mtu huacha yale mambo aliyozowea na matamanio yake kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na matokeo yake anachuma uchaji. Ni kama ambavo pia inavunja matamanio ya nafsi na nguvu zake. Kwa sababu shaytwaan hutembea ndani ya mwanadamu kama ambavo damu inatembea ndani ya mishipa. Shaytwaan anapata fursa ya kushambulia wakati mtu anapojiingiza ndani ya matamanio. Lakini akiacha mambo ya matamanio basi mishipa ya damu inakuwa dhaifu na hivyo shaytwaan anamkimbia muislamu. Kwa hiyo kumcha Allaah kunapatikana kupitia kufunga.

Hii ndio faida ya swawm ya kwamba inasababisha kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala), kujiepusha na mambo ya haramu na matamanio ya haramu. Kwa sababu mtu akiacha mambo ya halali kwa ajili ya kumtii Allaah basi anakuwa na wepesi zaidi wa kujiepusha na mambo ya haramu. Swawm inamzoweza mtu kujiepusha na haramu, inamzoweza kuimakinisha nafsi yake ambayo ni yenye kuamrisha maasi kwa wingi, pia inamfukuza mbali shaytwaan na inaulainisha moyo wake kufanya matendo mema. Ndio maana utamuona mtu aliyefunga anakuwa karibu zaidi na kheri kuliko ambaye hakufunga. Utamuona anapupia kusoma Qur-an, kuswali na kwenda msikitini mapema. Swawm ndio imemlainisha kufanya matendo mema. Yote haya yanaingia katika maneno Yake:

لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“”… ili mumche.”

Kinacholengwa katika Aayah ni maneno Yake:

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَام

“Mmefaradhishiwa swawm… “

Hii ni dalili juu ya ulazima wa funga. Imefasiriwa kwa maneno Yake:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ َ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan.”[3]

Mpaka aliposema:

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَام

“Mmefaradhishiwa swawm… “

Aayah iliyokuja kwa jumla imefasiriwa kwa maneno Yake:

 فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”[4]

[1] 02:183

[2] 02:216

[3] 02:185

[4] 02:185

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 190-192
  • Imechapishwa: 19/01/2021