Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

72 – Agano ambalo Allaah amelichukua kutoka kwa Aadam na kizazi chake ni haki.

MAELEZO

Bi maana fungamano ambalo Allaah (Ta´ala) amelichukua kutoka kwa Aadam na kizazi chake wamwabudu na wasimshirikishe na chochote ni haki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah alifunga mkataba kutoka kwenye mgongo wa Aadam. Baada ya kizazi chake chote kutoka mgongoni mwake akawatawanyisha mbele ya mikono Yake na akasema: “Je, mimi si Mola wenu?” Wakasema: “Ndio.”[1]

Ahadi hiyo inamaanisha wamwabudu Allaah na wasimshirikishe na chochote. Tunaiamini, lakini agano hilo halitoshi. Bali ilikuwa ni lazima pia kuwatumiliza Mitume, jambo ambalo Allaah amelifanya. Ingelikuwa agano hilo peke yake linatosha basi Allaah asingewatumiliza Mitume, lakini amewatumia Mitume ili wawakumbushe na wawalinganie watu katika yale yanayopatikana ndani ya agano hilo. Wako wanazuoni ambao wanasema kuwa agano hilo ni ile ambayo Allaah (Ta´ala) amesema juu yake:

وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖقَالُوا بَلَىٰ

“Na pindi Mola wako alipochukua katika wana wa Aadam kutoka migongoni mwao kizazi chao na akawashuhudisha juu ya nafsi zao: “Je, Mimi siye Mola wenu?” Wakasema: “Ndiye.”[2]

Mambo sivyo, hicho ni kitu kingine. Wanazuoni wengine wanaona kuwa agano hilo ni yale maumbile ambayo Allaah amewaumba juu yake na zile alama za kilimwengu ambazo amewaonyesha ili wapate kutambua kwazo Mola wao. Allaah (Subhaanah) amemuumba mwanadamu katika maumbile ya kumwabudu Yeye pekee na kujisalimisha Kwake:

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚلَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Basi elekeza uso wako katika dini yenye imani safi na iliyotakasika, imani hiyo ndio maumbile Allaah aliyowaumbia watu [wote] – hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah! Hivyo ndio dini iliyonyooka sawasawa, lakini watu wengi hawajui.”[3]

Huo ni Uislamu na Tawhiyd. Uislamu ni kule kumpwekesha Allaah ambako kumeletwa na Mitume na maana yake ni kumwabudu Allaah Mmoja pekee asiyekuwa na mshirika. Hii ndio dini ilionyooka imara. Ukiongezea zile dalili zinazothibitisha uola Wake na yale wanayoyaona katika nafsi zao wenyewe katika maumbile yao ya kushangaza, dalili nyinginezo za ajabu zinazojulisha juu ya Muumba. Amewaonyesha mbingu na ardhi zinazofahamisha juu ya Muumba. Viumbe hivi ni lazima viwe na Muumba, kwa sababu haiwezekani vikawa vimepatikana kwa bahati mbaya au pasi na Muumba:

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ  أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.”[4]

Ajabu iliyoje ni vipi anaasiwa Mungu

au ni vipi anakanushwa na mkanushaji

katika kila kitu kuna dalili

inayofahamisha kuwa Yeye ni Mmoja

Kila kilichoko mbele yako kinajulisha upwekekaji wa Allaah na kwamba amepwekeka katika kuumba viumbe hawa:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ ضُرِبَ مَثَلٌ فَاسْتَمِعُوا لَهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ

“Enyi watu! Imepigwa mfano basi isikilizeni kwa makini! Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah hawawezi kuumba nzi japo wakijumuika kwa hilo.”[5]

Muumba ni Allaah (Subhaanah). Hakuna mwingine anayeumba pamoja Naye. Vipi mtu atamwabudu mwingine ambaye haumbi, haruzuku na wala hamiliki juu ya nafsi yake manufaa wala madhara? Kwa hiyo maana ya Aayah:

وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ َ

“Wakati Mola wako alipochukua katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao na akawashuhudisha juu ya nafsi zao: “Je, Mimi siye Mola wenu?” Wakasema: “Ndio bila shaka.””[6]

ni ushuhuda wa maumbile na viumbe juu ya upwekekaji wa Allaah ili asiwepo yeyote atakayetoa udhuru siku ya Qiyaamah na kusema:

وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ

“Wakati Mola wako alipochukua katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao na akawashuhudisha juu ya nafsi zao: “Je, Mimi siye Mola wenu?” Wakasema: “Ndio bila shaka, tumeshuhudia [ili] msije kusema Siku ya Qiyaamah “hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya.”[7]

Haitofaa kujengea hoja kufuata kichwa mchunga mbele ya hoja za kukata kabisa na dalili za uhakika.

[1] al-Bayhaqiy katika ”al-Asmaa’ was-Swifaat” (714), Ahmad (1/172) na Ibn Abiy ´Aaswim (202).

[2]7:172

[3]30:30

[4]52:35-36

[5]22:73

[6]7:172

[7]7:172

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 102-105
  • Imechapishwa: 28/10/2024