90. Inajuzu kumtaka msaada mtu ambaye ni muweza na yuko mbele yako

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Wana hoja tata nyingine. Nayo ni kisa cha Ibraahiym alipotumbukizwa ndani ya Moto, Jibriyl akamfunulia na kusema: “Je, una haja ya kitu?” Akasema Ibraahiym: “Ama kama ni kutoka kwako, hapana.” Wanasema: “Lau kama ingekuwa kuombwa msaada Jibriyl ni shirki, asingejionesha kwa Ibraahiym.” Jibu ni: “Kwa hakika hii ni kama ile shubuha ya kwanza. Kwa hakika Jibriyl alijionyesha kwake ili amnufaishe kwa kitu ambacho anakiweza, kwani hakika yeye ni kama Allaah alivyomzungumzia:

شَدِيدُ الْقُوَىٰ

“Mwenye nguvu kabisa.” (53:05)

Lau Allaah angelimruhusu kuchukua moto wa Ibraahiym, ardhi na milima na kuvitupa mashariki au magharibi, angelifanya hivyo. Na lau Alingelimuamrisha kumuweka Ibraahiym (´alayhis-Salaam) mahali ambapo ni mbali na wao, angelifanya hivyo. Na lau Angelimuamrisha kumpandisha mbinguni, angelifanya. Huu ni kama mfano wa mtu tajiri ana mali nyingi na ameona mtu mwenye kuhitajia. Akajitolea kumpa mkopo au kumpa kitu atatue kwazo haja yake. Lakini yule mwenye kuhitajia akakataa kuzichukua na akasubiria Allaah kumpa riziki yake mwenyewe. Hili lina mafungamano yepi na kuomba msaada katika ´ibaadah na shirki, lau wangelikuwa wanafahamu?

MAELEZO

Hoja tata hii inaraddiwa ifuatavyo:

Jibriyl alijionyesha kwake ili amnufaishe kwa kitu ambacho anaweza kukifanya. Lau kama Allaah angemruhusu Jibriyl kumuokoa Ibraahiym kwa msaada wa nguvu ambazo Allaah (Ta´ala) amempa, basi angelifanya hivo. Allaah (Ta´ala) amemuelezea Jibriyl ifuatavyo:

شَدِيدُ الْقُوَىٰ

“Mwenye nguvu kabisa.”

Lau Allaah angelimruhusu kuchukua moto wa Ibraahiym, ardhi na milima na kuvitupa mashariki au magharibi, angelifanya hivyo. Na lau Alingelimuamrisha kumuweka Ibraahiym (´alayhis-Salaam) mahali ambapo ni mbali na wao, basi angelifanya hivyo. Na lau Angelimuamrisha kumpandisha mbinguni, basi angelifanya hivyo.

Halafu mtunzi akatoa mfano. Mtu ambaye ni tajiri na ni muweza akamwambia fakiri:

“Unahitajia pesa? Unahitajia mkopo? Unahitajia zawadi au kitu kingine?”

Hili ni jambo ambalo mtu huyu anaweza kufanya. Isingelizingatiwa shirki lau mtu huyo atakubali mambo haya.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 99-100
  • Imechapishwa: 28/11/2023