90. Kukutana na Allaah ni jambo lisiloepukika

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Yule ambaye atakabidhiwa daftari lake kwa mkono wa kuume, basi atafanyiwa hesabu nyepesi. Yule ambaye atakabidhiwa daftari lake nyuma ya mgongo wake, basi hao watachomwa Motoni.

MAELEZO

Kama alivosema Allaah (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَىٰ رَبِّكَ كَدْحًا فَمُلَاقِيهِ

“Ee mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa bidii kumwendea Mola wako, basi utakutana Naye.”[1]

Ni lazima ukutane na Allah (Subhaanahu wa Ta´ala). Wakati wa kukutana na Allaah watu wamegawanyika mafungu mawili:

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا وَيَنقَلِبُ إِلَىٰ أَهْلِهِ مَسْرُورًا

“Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atahesabiwa hesabu nyepesi na atageuka kwa ahli zake hali ya kuwa ni mwenye kufurahi.”[2]

Ataondoka kuelekea Peponi na wakazi wake hali ya kuwa ni mwenye furaha kutokana na yale aliyompa Allaah.

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاءَ ظَهْرِهِ فَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًا وَيَصْلَىٰ سَعِيرًا

“Ama yule atakayepewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake, ataomba kuteketea na ataingia achomeke moto uliowashwa vikali mno.”[3]

Atatwezwa na kupewa daftari lake kwa mkono wake wa kushoto kwa upande wa nyuma ya mgongo wake hali ya kuwa ni mwenye kuomba maangamivu.

إِنَّهُ كَانَ فِي أَهْلِهِ مَسْرُورًا

“Hakika yeye alikuwa katika ahli zake mwenye kufurahi.”[4]

Duniani alikuwa ni mwenye kufurahikia ladha na matamanivu ya dunia na huku akaisahau Aakhirah na asiifanyie kazi. Namna hii ndivo zilivyo hali nzito za watu siku ya Qiyaamah. Kwa yakini kabisa watakutana nazo.

[1] 84:6

[2] 84:7-9

[3] 84:10-12

[4] 84:13

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 68-69
  • Imechapishwa: 24/08/2021