89. Usiku ambao kunapambanuliwa mambo yote ya ndani ya mwaka

Ndugu! Ndani ya nyusiku hizi kumi kuna usiku wa makadirio ambao Allaah ameutukuza kuliko nyusiku nyenginezo na Allaah akautunuku ummah huu kwa fadhilah na kheri zake nyingi zaidi. Allaah amesifu fadhilah zake ndani ya Kitabu Chake kinachobainisha pale aliposema:

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ أَمْرًا مِّنْ عِندِنَا ۚ إِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ إِن كُنتُم مُّوقِنِينَ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ رَبُّكُمْ وَرَبُّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ

”Hakika Sisi tumeiteremsha katika usiku uliobarikiwa – hakika Sisi tumekuwa [daima ni] wenye kuonya [watu] – Humo [katika usiku huo] hupambanuliwa kila jambo la hikmah na jambo [Tunalokadiria ni lenye] kutoka Kwetu – hakika Sisi [daima] ndio wenye kutuma [wajumbe Wetu kwa mafunzo na mwongozo]. – Ni Rahmah kutoka kwa Mola wako, hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. Mola wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake mkiwa ni wenye yakini. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, anahuisha na kufisha. Ni Mola wenu na Mola wa baba zenu wa mwanzo.”[1]

Allaah (Subnaanah) ameeleza kuwa ni wenye baraka kutokana na kheri, baraka na fadhilah zake nyingi.

Miongoni mwa baraka zake ni kwamba Qur-aan hii tukufu imeteremshwa ndani yake. Ameeleza (Subhaanah) kwamba hupambanua ndani yake kila jambo lenye hekima. Kwa maana ya kwamba hutenganisha kutoka katika Ubao uliohifadhiwa na kuyaweka ndani ya kitabu yatayokuwepo katika amri za Allaah katika mwaka huo kukiwemo riziki, muda wa kueshi, mambo ya kheri, mambo ya shari na mengineyo. Hukadiriwa kila jambo lenye hekima katika amri za Allaah kamili ambazo ndani yake hakuna mapunfugu yoyote – hayo ni makisio ya Mwenye nguvu aliyeshinda, Mjuzi wa kila jambo. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ

“Hakika Sisi Tumeiteremsha katika usiku wa Qadar. Na nini kitakachokujulisha ni nini huo usiku wa Qadar? Usiku wa cheo ni mbora kuliko miezi elfu; wanateremka humo Malaika na Roho kwa idhini ya Mola wao kwa [ajili ya kutekeleza] kila jambo [Lake]. [Usiku huo kunakuwa na] amani mpaka kuchomoza alfajiri!”[2]

Neno (الْقَدرُ) maana yake ni cheo na utukufu au maana yake ni makadirio na mipango. Usiku wa makadirio ni wenye utukufu na mkubwa ambapo Allaah hukadiria na hupanga humo yatayokuwa ndani ya mwaka katika mambo ya hekima:

لَيْلَةِ الْقَدْرِ

”Usiku wa Qadar.”

Bi maana kwa ubora, utukufu na wingi wa thawabu. Kwa ajili hiyo ndio maana ikawa kwa yule ambaye atasimama kwa imani na kwa kutarajia malipo, basi husamehewa madhambi yake yaliyotangulia:

تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا

”… wanateremka humo Malaika na Roho… ”

Malaika ni waja miongoni mwa waja wa Allaah. Wanasimamia ´ibaadah za Allaah usiku na mchana:

لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لَا يَفْتُرُونَ

”Hawatakabari na ‘ibaadah Yake na wala hawachoki. Wanasabihi usiku na mchana wala hawazembei.”[3]

Hushuka katika usiku wa makadirio ulimwenguni wakija na kheri, baraka na rehema:

وَالرُّوحُ

”… na Roho… ”

Ni Jibriyl (´alayhis-Salaam). Ametajwa peke yake kutokana na utukufu na ubora wake.

سَلَامٌ هِيَ

”… [Usiku huo kunakuwa na] amani… ”

Bi maana usiku wa makadirio ni usiku wa salama kwa waumini kutokana na kila khofu kwa sababu ya wengi ambao wanaachiwa huru na Moto na kusalimishwa na adhabu yake:

حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ

”… mpaka kuchomoza alfajiri!”

Bi maana usiku wa makadirio unaisha kwa kupambazuka alfajiri kwa kumalizika matendo yake ya usiku.

[1] 44:03-08

[2] 97:01-05

[3] 21:19-20

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 159-161
  • Imechapishwa: 15/03/2024