2 – Uombezi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu watu wa Peponi waingie Peponi. Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye wa kwanza ambaye atafungua mlango wa Peponi, yeye ndiye wa kwanza atakayeingia na ummah wake ndio wa mwanzo watakaoingia[1].

3 – Uombezi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu watu wa Peponi zinyanyuliwe ngazi zao ambapo Allaah atamkubalia maombi yake.

4 – Uombezi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa waislamu watenda madhambi makubwa ambao wanastahiki kuingia Motoni wasiingie, na wale ambao wamekwishaingia watoke humo. Uombezi huu ndio wenye makinzano. Jahmiyyah, Khawaarij na vifaranga vyao wameupinga na kusema kuwa mwenye kuingia Motoni basi hatotoka humo. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameithibitisha na kuiamini kama ilivyokuja. Ni wajibu kwa muislamu kuiamini na amwombe Allaah kumfanya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuombea, kwa sababu ataihitaji. Isitoshe ni kwamba wako wengine ambao watakuwa na haki ya uombezi huu. Malaika, Mitume na mawalii na waja wema watawaombea watenda madhambi makubwa. Watoto waliokufa kabla ya kubaleghe watawaombea wazazi wao.

5 – Uombezi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuombea ami yake Abu Twaalib. Abu Twaalib alikufa katika shirki na katika dini ya ´Abdul-Muttwalib. Kwa ajili hiyo akawa ni miongoni mwa watu ambao watadumishwa Motoni milele. Hata hivyo Allaah atamwacha Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amwombee apunguziwe adhabu. Atakuwa katika ule Moto usiyokuwa wa kina. Ataona kuwa hakuna mtu mwenye adhabu kali kumshinda, licha ya kuwa yeye ndiye mtu wa Motoni mwenye adhabu ndogo kabisa.

[1] Muslim (196).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 100-102
  • Imechapishwa: 29/01/2023