89. Karibu ni zamu yako kulala ndani ya shimo

Itambulike kuwa uimirishaji wa waliohai na waliokufa sio kwa uinje. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah hatazami sura zenu wala miili yenu. Anachotazama ni nyoyo zenu.”

Uimirishaji wa moyo ndio uimirishaji wenye kunufaisha. Vivyo hivyo maiti ndani ya kaburi. Haihusiani na kuliremba kaburi na udongo. Uimirishaji wa kweli ni kwa kumtolea swadaqah na kumfanya matendo mema. Haya yameshatangulia katika milango iliyotangulia. Je, mtu hajui kuwa kaburi ambalo uinje wake limepambwa kwa ndani yake ni giza na lenye kubana? Ndani yake mtu amemtupa nduguye anayempenda sana na kumwacha akalala peke yake bila ya mto wala shuka. Juu yake amefunikwa na udongo na anafikwa na unyevu. Ameyaacha maisha ya duniani nyuma yake na kukitupa kila alichokuwa amekishika mkononi. Mpenzi wake amemwacha. Ndugu zake wamemwacha. Ndugu! Yote haya niliyokutajia yanakata ile ladha na matamanio. Lililo muhimu zaidi ni kuimirisha ule uinje kuliko ule undani, nao ni ule uimirishaji wenye kunufaisha siku ya Qiyaamah. Lau utazingatia kikweli na kwa makini basi utaona kuwa karibu ni zamu yako kwenda kule alikoenda mwenzako. Wakati mja yuko anacheza na kughafilika na siku yake ya kufa tahamaki humfika mauti. Sitara yake inafichuka. Nuru yake inazima. Athari yake inapotea. Kifo kimemtoa nje ya ikulu yake na nyumba yake nzuri na kumwingiza kwenye shimo kama shimo la ndugu yake, mtoto wake au mtu mwingine. Mashimo hayo yana giza na ni yenye kubana. Yamejaa woga na mfazaiko. Hakika kaburi ima ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi au ni shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni – Allaah atukinge nayo.

Baadhi ya wenye kuipa nyongo dunia waliulizwa ni yepi mawaidha bora kabisa. Wakasema:

“Kuyatazama makaburi.”

Ikiwa ni mawaidha kuyatazama makaburi ambayo ndio kituo cha kwanza cha Aakhirah na ni mazingatio kwa waliohai hayatakiwi kapambwa wala kurembwa. Wala haitakiwi kufanya yale yanayofanywa na wengi katika watawala, wafanya biashara na wengineo pale wanapotandika kwenye makaburi yao mahema, mikeka, magodoro na vinginevyo ambavyo wanalalia juu yake ilihali ndugu zao wamelala chini ya udongo kwenye mashimo ya kujibana na yenye giza. Ni mazingatio gani hawa wamepata kwa maiti wao? Huku ni kughafilika. Tunamuomba Allaah atusalimishe nayo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 190-191
  • Imechapishwa: 01/12/2016