Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Hadiyth kuhusu kutolewa kwa roho inasema:

“Wakati mtu anapokufa ikiwa mtu alikuwa mwema anajiwa na Malaika ambao wanasema: “Toka, ee nafsi nzuri iliokuwa kwenye mwili mzuri. Toka ukiwa ni mwenye kusifiwa na pata bishara njema ya rehema, mimea yenye harufu nzuri na Mola si Mwenye kukasirika.” Kutaendelea kusemwa hivo mpaka pale inapotoka. Halafu ipandishwe juu mbinguni. Itaombewa idhini ya kuingia ambapo kutasemwa: “Ni nani huyu?” Kutasemwa kwamba ni fulani ambapo watasema: “Karibu, ee nafsi nzuri iliokuwa kwenye mwili mzuri. Ingia ukiwa ni mwenye kusifiwa na pata bishara njema ya rehema, mimea yenye harufu nzuri na Mola si Mwenye kukasirika.” Hakutoacha kuendelea kusemwa hivo mpaka ifike kwenye mbingu ambayo Allaah (´Azza wa Jall) Yuko juu yake.”[1]

Cheni ya wapokezi wake ni kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.

MAELEZO

Wakati inapotolewa roho ya maiti, hupandishwa juu mbinguni. Ikiwa ni roho ya muumini, basi hupewa idhini kuzivuka mbingu na kufunguliwa milango yake. Hatimaye ikafika mpaka kwa Allaah ambapo Akasema (´Azza wa Jall):

”Irudisheni ardhini. Nimewaumba kutokana nao na nitawarudisha humo na kutokea humo nitawatoa tena kwa mara nyingine.”

Kuhusu kafiri, hatofunguliwa milango ya mbingu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا لَا تُفَتَّحُ لَهُمْ أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَلَا يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ حَتَّىٰ يَلِجَ الْجَمَلُ فِي سَمِّ الْخِيَاطِ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُجْرِمِينَ

“Hakika wale waliozikadhibisha Aayah Zetu na wakazifanyia kiburi, hawatofunguliwa milango ya mbingu na wala hawatoingia Peponi mpaka ngamia aingie katika tundu ya sindano – hivyo ndivyo Tunavyowalipa wahalifu.”[2]

Roho yake itarushwa kwa ukali ardhini na itafikwa na utwevu na udhalilifu. Baada ya hapo roho yake itapelekwa kwenye mashimo ya gereza. Allaah (Subhaanah) amesema:

”Kiandikeni kitabu cha mja Wangu kwenye mashimo ya gereza.”

Bi maana katika kina cha chini kabisa.

Kinachokusudiwa katika Hadiyth ni kwamba roho hupandishwa kwa Allaah, jambo ambalo linafahamisha kuwa Allaah yuko juu ya mbingu.

[1] Ibn Maajah (4262) na Ahmad (2/364). Swahiyh kwa mujibu al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (3456). adh-Dhahabiy amesema:

“Ameipokea Ahmad katika ”al-Musnad” na al-Haakim katika ”al-Mustadrak” ambaye amesema: ”Ni kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.” (al-´Uluww, uk. 22)

[2] 7:40

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 128-129
  • Imechapishwa: 26/08/2024