87. Miaka elfukhamsini katika joto kali na hali ya kutisha

Watu watakusanyika na wakiwa ni wenye kusimama kwa miguu yao, wakiwa uchi na pasi na kutahiriwa. Jua litawekwa karibu nao na wataanza kutokwa na majasho kutegemea na matendo yao. Hali yao itakuwa ngumu na ya kutisha kwelikweli. Amesema (Ta´ala):

مِّنَ اللَّـهِ ذِي الْمَعَارِجِ تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ خَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ

“Kutoka kwa Allaah Mwenye njia za kupandia. Malaika na Roho wanapanda Kwake katika siku kadiri yake ni miaka khamsini elfu.”[1]

Watasimama kwa muda wa miaka khamsini kwenye joto kali na msongamano. Watu wa zama zote. Hapo ndipo wataenda kwa ambaye anaweza kuwaombea mbele ya Allaah ili ahukumu baina yao na kuwapumzisha kutokamana na mkusanyiko. Matokeo yake wataenda kwa Aadam (´alayhis-Salaam), ambaye ni baba wa watu, watasema:

“Ee Aadam! Hakika wewe ndiye baba wa watu. Allaah amekuumba kwa mkono Wake, akakupulizia roho Yake na akawaamrisha Malaika kukusujudia. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Aadam atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Alinikataza kula katika mti ambapo nikamuasi. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Nuuh.” Waende kwa Nuuh na kusema: “Ee Nuuh! Wewe ndiye Mtume wa kwanza kutumilizwa ardhini. Allaah amesema kuwa wewe ni mja mwenye kushukuru. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Nuuh atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Nilikuwa na haki ya du´aa yenye kuitikiwa na nikaiomba dhidi ya watu wangu. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Ibraahiym.” Waende kwa Ibraahiym na kusema: “Ee Ibraahiym! Wewe ni kipenzi mwandani kabisa wa Allaah na Mtume Wake ardhini. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Ibraahiym atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake.” Atataja kusema kwake uongo mara tatu kisha atasema: “Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Muusa.” Waende kwa Muusa na kusema: “Ee Muusa! Wewe ni Mtume wa Allaah! Allaah amekuteua kutokamana na watu wengine wote kwa ujumbe na maneno Yake. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Muusa atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Niliua nafsi bila idhini. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa ´Iysaa.” Waende kwa ´Iysaa na kusema: “Ee ´Iysaa! Wewe ni Mtume wa Allaah. Uliwazungumzisha watu katika hali ya uchanga. Wewe ni neno Lake alilolirusha kwa Maryam na roho inayotokamana Naye. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” ´Iysaa atasema: “Hakika Mola wangu ameghadhibika ghadhabu ambayo kamwe hajapatapo kughadhibika na hatoghadhibika mfano wake baada yake. Nachelea juu ya nafsi yangu. Nendeni kwa mwingine, nendeni kwa Muhammad.” Waende kwa Muhammad na kusema: “Ee Muhammad! Wewe ni Mtume wa Allaah na Nabii wa mwisho. Allaah amekusamehe dhambi zako zote. Tuombee kwa Mola wako! Kwani huoni yale tuliyomo?” Nitaondoka mpaka nitakapofika chini ya ´Arshi ambapo nitasujudu mbele ya Mola wangu. Kisha Allaah ataniidhinisha kumhimidi kwa njia ambayo hajapatapo kuhimidiwa na mwingine yeyote. Ataambiwa: “Ee Muhammad! Inua kichwa chako. Uliza utapewa, omba utapokelewa uombezi wako.” Nitainua kichwa changu na kusema: “Ee Allaah! Ummah wangu! Ummah wangu!” Kutasemwa: “Ee Muhammad! Wale ambao katika Ummah wako ambao hawatofanyiwa hesabu waingize Peponi kupitia milango yake ya kulia. Milango mingine yote ya Peponi watashirikiana na wengineo.” Naapa kwa Yule ambaye mkononi Mwake iko roho yangu umbali kati ya milango miwili ya Pepo ni kama umbali kati ya Makkah na Hajar, au ni kama umbali kati ya makkah na Busraa.”[2]

[1] 70:03-04

[2] al-Bukhaariy (7510) och Muslim (194).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 64-66
  • Imechapishwa: 23/08/2021