Ni sahihi kumpa muislamu aliyehai thawabu za ´ibaadah za Sunnah? Suala hili linakaribia kutokupatikana katika vile vitabu vinavyojulikana kutokana na ugeni wake. Ibn Tamiym amelitaja katika kitabu chake na kusema kuwa thawabu zinamfikia yule maiti na Hanaabilah wana maoni mawili kama zinamfikia aliyehai pia.

Baadhi ya Hanafiyyah watukufu wamenieleza kuwa thawabu zinamfikia aliyehai kwa mujibu wa madhehebu yao. Dalili ya hilo ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ

“Basi wasamehe na waombee msamaha.” 03:159

Isitoshe Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) na waislamu kwa jumla hawakuacha daima kuombeana du´aa wao kwa wao, waliokufa na waliohai, pasi na yeyote kuwakataza kitendo hicho. Imewekwa katika Shari´ah kusema katika du´aa ya kumuombea maiti:

“Ee Allaah! Wasamehe waliohai wetu na maiti wetu.”

al-Qaadhwiy Abu Ya´laa amesema:

“Haijulikani kuwa Imaam Ahmad anatofautisha kati ya aliyehai na maiti. Udhahiri ni kuwa maoni yake yanahusu wote wawili. Ni jambo linalothibitishwa na Qur-aan na Sunnah katika du´aa na kuwaombea msamaha wote wawili. Hakuna tofauti. Shaykh Shams-ud-Diyn bin ´Abdil-Qawiy amesema katika “Majm´-ul-Bahrayn”:

“Hakuna anayepinga hilo. Kuna maafikiano juu ya hilo. Mwenye kusema kuwa haijuzu hana utata.”

Ibn ´Aqil amesema katika “al-Mufradaat”:

“Kisomo cha Qur-aan na mfano wa hayo hayamfikii aliyehai. Ni jambo linafungua mlango wa madhara makubwa. Linapelekea kwa wale matajiri kuacha kufanya matendo kwa kutoa pesa tu kuwapa ambao wanaweza kuwafanyia matendo. Matokeo yake wanakosa thawabu kwa kutegemea thawabu za wengine na ´ibaadah inabadilishwa kwa kitu mbadala.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 187-188
  • Imechapishwa: 29/11/2016