87. Hali tatu kwa anayefanya I´tikaaf kutoka nje ya msikiti

Kuna hali tatu kwa mwenye kufanya I´tikaaf akahitaji kutoka nje ya msikiti:

1 – Kutoka kwa ajili ya jambo ambalo limemlazimu. Jambo hilo linaweza kuwa la kimaumbile au kwa mujibu wa Shari´ah. Kwa mfano akatoka kwa ajili ya kukidhi haja ndogo, haja kubwa, kutawadha ambako ni wajibu, josho la wajibu kutokana na janaba na mengineyo kama vile kula na kunywa. Inafaa ikiwa hawezi kuyafanya mambo hayo msikitini. Akiweza kuyafanya msikitini haitofaa kutoka. Kwa mfano msikitini kukawepo choo kinachomuwezesha kufanya kukidhi haja yake na kuoga. Mfano mwingine akawepo mtu anayeweza kumletea chakula na kinywaji. Katika hali hiyo hatoruhusiwa kutoka kwa sababu hakuna haja ya hilo.

2 – Kutoka kwa ajili ya jambo la kitiifu ambalo sio wajibu kwake. Mfano wa mambo hayo ni kumtembelea mgonjwa na kuhudhuria mazishini. Asifanye mambo hayo. Isipokuwa kama atashurutishiwa mambo hayo mwanzoni mwa I´tikaaf yake. Kwa mfano yuko na mgonjwa ambaye atapendelea kwenda kumtembelea au anachelea kufa kwake. Hivyo hapana vibaya akaweka sharti mwanzoni mwa I´tikaaf yake kwamba atatoka kwenda kumtembelea.

3 – Kutoka kwa ajili ya jambo linalopingana na I´tikaaf yake. Mfano wa mambo hayo ni kutoka kwa ajili ya kufanya biashara, kumjamii na kujichanga na mke wake na mfano wake. Asifanye mambo hayo; ni mamoja aliweka sharti au hakuweka sharti. Kwa sababu jambo hilo linapingana na I´tikaaf na pia linapingana na malengo yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 157-158
  • Imechapishwa: 13/03/2024