Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hali kadhalika Hadiyth nyingine na mfano wake. Maana yake ni [haya] tuliyoyasema; ya kwamba mwenye kudhihirisha Tawhiyd na Uislamu basi ni wajibu kukomeka naye isipokuwa ikibainika kutoka kwake yanayokhalifu hilo. Dalili ya hili ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kasema:

“Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah?””

Kadhalika amesema:

“Nimeamrishwa kupigana na watu mpaka waseme “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah”.”

Kasema kuhusu Khawaarij:

“Popote mtapokutana nao waueni. Lau nitakutana nao, nitawaua kama walivyouawa kina ´Aad.”

Haya pamoja na kwamba ni katika watu wenye kufanya ´ibaadah, walikuwa wakisema hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na wakimsabihi Allaah kwa wingi. Mpaka hata Maswahabah walikuwa wakizidharau swalah zao wakilinganisha na zao. Pia wamejifunza elimu kutoka kwa Maswahabah. Hata hivyo “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” haikuwafaa kitu, wala wingi wa ´ibaadah wala kudai kwao Uislamu pindi ilipodhihiri kwao kukhalifu kwao Shari´ah.

MAELEZO

Hadiyth nyingine anamaanisha maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kupigana na watu mpaka waseme “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah”.”

Amebainisha (Rahimahu Allaah) ya kuwa maana ya Hadiyth ni kwamba ni wajibu kukomeka na ambaye anadhihirisha Uislamu mpaka jambo lake libainike. Amesema (Ta´ala):

فَتَبَيَّنُوا

“… basi thibitisheni.” (04:94)

Ikiwa tuna shaka kwa mtu, tunahitajia kuhakikisha. Vinginevyo ni kwamba lau kusema kwake ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaa` ingelikuwa ni kwa sababu tu ya kutaka kusalimika na kifo, basi kungelikuwa hakuna haja ya kuhakikisha.

Baada ya hapo mtunzi (Rahimahu Allaah) akathibitisha maoni yake ya kwamba ambaye alimwambia Usaamah “Hivi kweli umemuua baada ya yeye kusema “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah?”” na “Nimeamrishwa kupigana na watu mpaka waseme “Hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah”.”, ndiye mtu huyohuyo aliyeamrisha kuwapiga vita Khawaarij pale alposema:

“Popote mtapokutana nao waueni. Lau nitakutana nao, nitawaua kama walivyouawa kina ´Aad.”[1]

Haya pamoja na kuwa Khawaarij wanaswali, wanamdhukuru Allaah na kusoma Qur-aan. Wamesoma kutoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Licha ya hivyo hayakuwafaa kitu, kwa sababu imani katu haikufika ndani ya nyoyo zao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kwa hakika haivuki koo zao.”[2]

[1] al-Bukhaariy (6930) na Muslim (1066).

[2] al-Bukhaariy (7432) na Muslim (1066).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 28/11/2023