86. Mapendekezo ya kumuombea maiti baada ya kuzikwa

Imaam Ahmad amesema kuwa imependekezwa kumuombea du´aa maiti moja kwa moja baada ya kuzikwa na kwamba ni jambo lilifanywa na ´Aliy bin Abiy Twaalib na al-Ahnaf bin Qays. Imepokelewa kutoka kwa ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa baada ya kumzika maiti anasimama karibu na kaburi lake na kusema:

“Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumtakie uthabiti. Kwani hakika hivi sasa atahojiwa.”

Ameipokea Abu Daawuud.

Vilevile ash-Shaafi´iy anaonelea kuwa imependekezwa kumuomba du´aa yule maiti moja kwa moja baada ya kuzika.

Wafasiri wengi wa Qur-aan wanasema maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) juu ya wanafiki:

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ

“Na wala usimswalie yeyote kamwe katika wao akifa na wala usisimame kwenye kaburi lake.” 09:84

inahusu kumuombea du´aa na msamaha baada ya kuzikwa. Kundi la wafasiri wa Qur-aan wanasema kuwa pindi Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) alipotaka kumuombea msamaha ami yake Abu Twaalib baada ya kufa kwake na pindi Maswahabah walipotaka kuwaombea msamaha baba zao ndipo Allaah (Ta´ala) akateremsha:

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ

“Haimpasi Nabii na wale walioamini kuwaombea msamaha washirikina, japokuwa ni jamaa zao wa karibu, baada ya kuwabainikia kwamba wao ni watu wa Motoni.” 09:113

Du´aa za waumini zingelikuwa hazinufaishi basi Aayah hizi zingelikuwa hazina maana yoyote. Alipokataza kuwaombea du´aa washirikina ni dalili inayofahamisha kuwa inawanufaisha waumini. Muhammad bin Habiyb at-Tammaar amesema:

“Nilikuwa na Ahmad bin Hanbal mazishini. Akanishika mkono na tukasimama pembezoni. Watu walipomaliza kumzika yule maiti tukaliendea kaburi lile. Akakaa chini na kuweka mkono wake juu ya kaburi. Kisha akasema: “Ee Allaah! Hakika umesema katika Kitabu Chako:

فَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُقَرَّبِينَ

“Ama [yule anayefariki] akiwa miongoni mwa waliokurubishwa [kwa Allaah]… ” 56:88

akasoma Aayah yote. Halafu akasema: “Ee Allaah! Tunashuhudia kuwa mtu huyu hakukukadhibisha na kwamba alikuamini na Mtume Wako. Ee Allaah! Tunakuomba utukubalie ushahidi wetu juu yake.” Halafu akamuombea na kwenda zake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 185-186
  • Imechapishwa: 27/11/2016