85. Mwenye kutamka Shahaadah anasalimishwa maadamu hakujathibiti kinyume

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Lakini maadui wa Allaah hawakufahamu maana ya Hadiyth hizo. Ama Hadiyth kuhusu Hadiyth ya Usaamah, alimuua mtu ambaye alidai Uislamu kwa sababu alidhani ya kwamba anadai Uislamu kwa khofu tu ya kuuliwa na mali yake. Na mtu akidhihirisha Uislamu, basi ni wajibu kukomeka naye mpaka ibainike yanayokhalifu hilo. Allaah kateremsha kuhusiana na hilo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا ضَرَبْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَتَبَيَّنُوا

“Enyi mlioamini! Mnaposafiri [kupigana jihaad] katika njia ya Allaah thibitisheni.” (04:94)

Bi maana hakikisheni. Aayah inatoa dalili ya kwamba ni wajibu kukomeka naye mpaka mtu ahakikishe. Baada ya muda kukibainika kutoka kwake yanayokhalifu Uislamu, anauawa, kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

فَتَبَيَّنُوا

“… thibitisheni.”

Na lau ingelikuwa hauawi akitamka [Shahaadah], kuhakikisha kungekuwa hakuna maana yoyote.

MAELEZO

Hawafahamu Hadiyth hizi ambazo wamezifahamu kimakosa. Halafu baada ya hapo akaanza (Rahimahu Allaah) kuzibainisha na kusema:

Kuhusiana na Hadiyth ya Usaamah ambapo mshirikina aliyesema “Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” baada ya kumdhibiti, Usaamah akamuua kwa kudhani ya kwamba hakuisema kutoka moyoni. Alidhani kuwa alisema hivo kwa sababu ya woga. Hapa hakuna dalili yoyote ya kwamba kila mwenye kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` ni muislamu ambaye damu yake ni haramu kumwagwa. Lakini kuna dalili ya kwamba ni wajibu kukomeka na yule mwenye kusema hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Baada ya hapo kutatazamwa hali yake mpaka mambo yabainike. Mtunzi akajengea dalili ya hilo kwa maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا ضَرَبْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَتَبَيَّنُوا

“Enyi mlioamini! Mnaposafiri [kupigana jihaad] katika njia ya Allaah thibitisheni.”

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ameamrisha kuhakikisha na kuthibitisha. Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa ikiwa mambo yanaenda kinyume na hali yake, atataamiliwa kwa mujibu wa hali yake ya dhahiri. Kukibainika kwake yenye kwenda kinyume na Uislamu, anauawa. Endapo asingeliuawa kabisa kwa maneno kama hayo, basi kusingelikuwa na faida yoyote ile ya maamrisho ya kuhakikisha.

Hivyo Hadiyth ya Usaamah (Radhiya Allaahu ´anh) haifahamishi kwamba yule mwenye kusema ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na huku anaabudia masanamu, maiti, Malaika, majini na mfano wake anakuwa muislamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 92-93
  • Imechapishwa: 28/11/2023