Swali 84: Je, una lolote la kusema kuhusu mkusanyiko, kusikiliza na kutii?

Jibu: Allaah ameuamrisha ummah wa Kiislamu kukusanyika juu ya haki na akawakataza kugawanyika na kutofautiana. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane!”[1]

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا

“Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakakhitilafiana.”[2]

Amewaamrisha (Subhaanah) kusuluhisha yaliyo kati yao wakati kunapotokea tofauti na akasema:

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Ikiwa makundi mawili ya waumini yatapigana, basi suluhisheni baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee katika amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni kati yao kwa uadilifu na tendeni haki. Kwani hakika Allaah anawapenda wanaotenda haki. Hakika mambo yalivyo ni kwamba waumini ni ndugu, hivyo basi suluhisheni kati ya ndugu zenu na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.”[3]

Ni jambo linalotambulika kuwa waislamu hawawezi kuwa na umoja wala kukusanyika isipokuwa kwa kuwepo uongozi mwema ambapo utamshughulikia yule mwenye kudhulumu na kumtendea haki yule mwenye kudhulumiwa. Uongozi unatakiwa kuitetea nchi yake, kuzitekeleza zile hukumu za Shari´ah na kulinda amani. Kwa ajili hiyo Ahl-us-Sunnah wameafikiana juu ya kwamba ni lazima kumteua kiongozi[4]. Wakati alipokufa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Maswahabah hawakumwandaa mpaka kwanza walipomteau kiongozi ambaye atachukua nafasi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo wakala kiapo cha utiifu kwa Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh). Hilo linafahamisha jinsi jambo hili lilivyo muhimu na kutolichukulia wepesi.

[1] 3:103

[2] 03:105

[3] 49:9-10

[4] Mambo yanakuwa namna hii hata kama mtawala huyo atakuwa fasiki. Hakika kusimamisha hukumu na Shari´ah ya Allaah ardhini ni jambo linampendeza zaidi kuliko jambo hilo kupuuzwa na kuwaacha watu hali ya mkanganyiko. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Adhabu iliyowekwa na Shari´ah inayofanyiwa kazi ardhini ni bora kwa watu walioko ardhini kuliko kunyesha mvua asubuhi arobaini.” (Tazama ”as-Swahiyhah” (231))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 210-211
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy